Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Sudan wengi zaidi nchini CAR, UNHCR yakimbizana na muda kuiwahi mvua  

Wakimbizi wa Sudan wakielekea nchi jirani.
© WFP/Jacques David
Wakimbizi wa Sudan wakielekea nchi jirani.

Wakimbizi wa Sudan wengi zaidi nchini CAR, UNHCR yakimbizana na muda kuiwahi mvua  

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu 13,000 kutoka Sudan wamewasili katika Kijiji cha Am Dafock kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kuepuka madhila ya mgogoro unaoendelea nchini mwao. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linasema wengi wa waliowasili ni wanawake na watoto kutoka Nyala mji ulioko kusini magharibi mwa Sudan ambako wanasema walikabiliwa na matatizo kadhaa njiani kuelekea kuvuka mpaka hadi kufika Am Dafock, kama vile vitisho kutoka kwa watu wenye silaha, unyang'anyi wa bidhaa, unyanyasaji wa kimwili na unyanyasaji wa kijinsia. 

Katika eneo kame la Am Dafock nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ni kadamnasi ya wakimbizi kutoka Sudan wameketi chini ya vivuli vya kuibiaibia kwani miti ni michache mno hapa.  

Soundcloud

Mmoja wa wakimbizi waliofika hapa kwa tabu ni Halima Hamid Adam, anasema, "Tulivuka mpaka kwa miguu na kutembea kwa kilomita nyingi, tulipofika kwenye barabara kuu tukamkuta mfanyabiashara aliyetuleta hapa kwa gari lake." 

Kulingana na hali mbaya ya hapa wakimbizi walipofikia, mmoja wa maafisa wa UNHCR ambao wanasimamia takwimu, Bwana Bobo Kitoko, akiwa hapa anasema, “Kwa hiyo watu hawa watahamishwa haraka na tunakimbizana na muda ili mvua isiwapate hapa Am Dafock. Vinginevyo, itakuwa ngumu." 

UNHCR na WFP wamekuwa wakisambaza misaada muhimu kama vile maji na chakula kwa wanaowasili. Unaonekana msusuru wa madumu wote ukielekea kwenye mkokoteni wa kukokotwa kwa farasi, kila mtu akitamani apate japo maji kidogo. Bobo Kitoko, Afisa wa UNHCR anarejea akisema, “Mahitaji ni mengi, kwa chakula, malazi na pia maji, na tunajaribu kuleta maji kutoka katika vyanzo tunavyoweza kupata hapa. Hii inamaanisha tunatumia mikokoteni ya farasi ambayo husafirisha matangi ya lita 400 za maji." 

Usajili wa kibayometriki pia ulianza mwezi uliopita na unaendelea. Ismaïl Ibrahim Mykaz Toto ambaye awali alikuwa anampepea mtoto kumpunguzia joto katika hema la usajili wakati mkewe aliyembeba mtoto akisajiliwa anasema, "Tulikuja hapa tukitafuta mahali pazuri. Ikiwa tutapata mahali pazuri, mahali salama, ndio, tutakaa hapo. Na pia hatujui wakati vita itakoma. Ndio maana tuliondoka. Hatujui itakoma lini. Ni mapigano makali sana.” 

UNHCR na wadau wake wanaunga mkono juhudi za serikali za kutoa huduma ya ulinzi linalozingatia mahitaji ya dharura ya wakimbizi wa Sudan wanaowasili Am-Dafock na mahitaji ya wakimbizi wa Afrika ya Kati wanaorejea nyumbani. Timu za dharura zinatambua na kuwaelekeza watu wenye mahitaji maalum ya ulinzi, ushauri au usaidizi wa matibabu. 

Operesheni kadhaa za dharura zimefanyika licha ya changamoto katika kufika eneo hilo, kutokana na umbali wake na hali tete ya usalama. 

Zaidi ya kaya 36 zimehamishwa hadi kwenye eneo salama ambapo familia zinaweza kupata huduma kwa urahisi. Kipaumbele cha uhamishaji kinatolewa kwa wakimbizi waliosajiliwa kibayometriki na walio hatarini zaidi. 

Kazi za ujenzi wa makazi zaidi ya familia, vyoo na bafu zinaendelea.