Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya wakimbizi wa CAR warejea nyumbani kutoka DRC kwa msaada wa UNHCR

Picha ya UN
OCHA/Yaye N. Sene.
Picha ya UN

Maelfu ya wakimbizi wa CAR warejea nyumbani kutoka DRC kwa msaada wa UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR wamesaidia mamia ya wakimbizi wanaoishi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC kurejea nyumbani nchini Jamhuri ya Afrika ya kati.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi, msemaji wa UNHCR, Babar Baloch amesema, zoezi hilo la kurejea kwa hiari kwa mara ya kwanza kutoka DRC kwa zaidi ya wakimbizi 172,000 ambao walilazimika kukimbia CAR tangu 2013 limefanyika Alhamisi.

Takriban wakimbizi 400 na mali zao wamerejea kwa malori na magari madogo yaliyoondoka kambi ya Mole kuelekea Zongo katika mkoa wa Ubangi Kusini, nchini DRC na kuendelea na safari yao kwa boti hadi mji mkuu wa CAR, Bangui.

Wengi wa wakimbizi hao wameishi nchini DRC kwa miaka mingi baada ya machafuko nchini CAR kuwalazimu kukimbia na kusaka hifadhi nchi jirani.

Programu hiyo ya kurejea kwa hiari ni kufuatia makubaliano ya utatu kati ya UNHCR, serikali ya DRC na ya CAR Juni 2019.

Bwana Baloch amesema tangu kutiwa saini kwa makubaliano hayo watu 4,000 wamejiandikisha kutaka kurejea nyumbani kufikia mwisho wa 2019 huku wengine wakifanya mipango yao wenyewe kurejeea. UNHCR inatarajia kusaidi watu 25,000 kufikia mwisho wa mwaka 2020 kupitia programu hiyo.

Wakimbizi wanaorejea wanapatiwa usafiri na mfuko maalum wa kurejea ulio na pesa taslimu za vifaa vya msingi vya matumizi nyumbani kwa ajili ya kuanza maisha nchini CAR.

UNHCR pia inawasaidia kujumuishwa tena katika jamii kwa kuwasaidia kupata stakabadhi muhimu kutoka serikalini na vyeti vya shule. Aidha shirika hilo wamejenga madarasa katika baadhi ya maeneo ambako wakimbizi wanarejea.

Msemaji huyo ameongeza kuwa wakimbizi wengi ambao ni wakulima wamepatiwa mashamba na serikali kwa ajili ya kulima chakula na kulisha familia zao. UNHCR pia inashirikiana na mamlaka za kisheria kwa ajili ya kuwezesha wakimbizi kupata mali zao walizopoteza. Hata hivyo CAR inahitaji msaada zaidi katika juhudi za kuimairsha huduma za afya, elimu na huduma nyingine za kijamii

Zaidi ya wakimbizi 600,000 kutoka CAR wanaishi nchini DRC na nchi jirani huku idadi kama hiyo ni wakimbizi wa ndani nchini humo.