Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano mapya yawafungisha virago watu 2,000 CAR na kuingia Chad:UNHCR 

Mwanamke aanza maisha mapya katika kambi ya Doholo nchini Chad baada ya kukimbia mapigano nchini CAR.
© UNHCR
Mwanamke aanza maisha mapya katika kambi ya Doholo nchini Chad baada ya kukimbia mapigano nchini CAR.

Mapigano mapya yawafungisha virago watu 2,000 CAR na kuingia Chad:UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Mapigano kati ya vikosi vya serikali na vikundi vya waasi kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yaliyozuka wiki iliyopita yamelazimisha zaidi ya raia zaidi ya 2,000 kuvuka mpaka na kutafuta hifadhi katika nchi jirani ya Chad, limesema shirika la Umoja wa Mastaifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. 

Akizungumza na waandishi wa Habari hii leo mjini Geneva Uswis msemaji wa shirika la UNHCR mjini Babar Baloch amesema "Watu wapya waliowasili Chad kutoka mkoa wa Kaga-Bandoro huko CAR wameziambia timu za UNHCR kwamba walmelazimika kukimbia mapigano. Pia wamethibitisha kwamba kukimbia kwao kumechangiwa pia na kuongezeka kwa vitendo vya vurugu, uporaji au unyang’anyi unaofanywa na vikundi vya waasi wakati vikosi vya serikali vilipokaribia vituo vya waasi hao.” 

Bwana Baloch ameongeza kuwa "Wakati watu walipokuwa wakitembea kuelekea mpakani, watu wengine kutoka Batangafo na Kabo, kwenye barabara ya kwenda Chad, walifuata nyayo kwa kuogopa mashambulizi. Na kufika Chad, ilibidi watu wavuke mto Grande Sido, wengine wakibeba mali zao chache kichwani.” 

Wakimbizi hao sasa wamepata hifadhi katika kijiji cha Gandaza na katika mji wa mpakani wa Sido, ingawa wengine lazima waamue kuvuka kuingia CAR kupata chakula au kunusuru mali zao zilizobaki.  

Nyumba, chakula, maji, pamoja na upatikanaji wa huduma za usafi wa mazingira na huduma za afya, ni mahitaji ya haraka zaidi ya wakimbizi hao. 

Zaidi ya wakimbizi 117,000 wa CAR wako nchi jirani tangu Desemba 

Hivi sasa Chad imewapokea wakimbizi 11,000 kati ya 117,000 wa CAR  ambao pia wengine wamekimbilia nchi  jirani, za Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Jamhuri ya Congo Brazaville , kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu, ambazo pia zilmewalazimisha watu 164,000 kuwa wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati 

Bwana Baloch amesema ikumbukwe kwamba mapigano kaskazini mwa CAR yameanza tena kwa sababu ya uasi wwa silaha kufuatia "uchaguzi uliogombaniwa" mwezi Desemba mwaka jana.  

Hali ambayo ilifanya mamia ya maelfu ya watu kuwa wakimbizi ndani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na nje ya mipaka, katika majimbo jirani ya Bangui. 

Lakini, utitiri huo umepungua sana tangu katikati ya mwezi Machi, baada ya "vikosi vya serikali na washirika wao kuteka tena ngome nyingi za waasi." Hali ambayo iliruhusu hata watu 37,000 waliokimbia makazi yao kurudi katika mikoa yao ya asili. 

"Hatahivyo watu hawa sasa wanahitaji msaada wa kujenga upya maisha yao," amesema msemaji wa UNHCR, akibainisha kuwa uwezo wa mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataiufa kukidhi mahitaji ya msingi ya wakimbizi wa ndani na wakimbizi wan je umepunguzwa sana na kutokana na ukosefu wa fedha na rasilimali. 

Mgogoro wa kibinadamu huko CAR ni moja wapo ya shughuli za UNHCR ambazo hazina fedha nyingi duniani, na ni asilimia 12% tu ya dola milioni 164.7 zinazohitajika sasa, ndio zilizopatikana licha ya kiwango cha kiwango kikubwa cha watu waliotawanywa.  

Wakati huo huo, karibu theluthi moja ya idadi ya watu nchini CAR sasa wametawanywa baada ya miaka kumi ya ukosefu wa utulivu.