Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo la KEN QRF 2 ni kuzuia uhalifu kabla haujatokea DRC - Luteni Kanali David Munoru 

Luteni Kanali David Munoru, Kamanda wa  kikosi cha KEN QRF 2 kutoka Kenya wanaohudumu chini ya MONUSCO nchini DRC.
MONUSCO
Luteni Kanali David Munoru, Kamanda wa kikosi cha KEN QRF 2 kutoka Kenya wanaohudumu chini ya MONUSCO nchini DRC.

Lengo la KEN QRF 2 ni kuzuia uhalifu kabla haujatokea DRC - Luteni Kanali David Munoru 

Amani na Usalama

Kwa miaka takriban 20, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamefanya kazi chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC -MONUSCO ili kuokoa na kubadilisha maisha katika hali tete ya kisiasa na kiusalama humo. Miongoni mwa vikosi vinavyosaidia amani nchini humo ni KEN QRF 2.  

KEN QRF 2 ni kikosi cha pili cha walinda amani kutoka Kenya cha kuchukua hatua za haraka kinachohudumu mjini Beni, Jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) chini ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, DRC-MONUSCO

Mjini Beni, mashariki mwa DRC Luteni Kanali David Munoru ambaye ni Kamanda wa  kikosi KEN QRF 2 kutoka Kenya anaeleza mchango ya kikosi chake katika kusongesha amani nchini DRC akisema, "Kwanza kabisa ningetaka kusema kwamba kile kikosi tuko nacho hapa ambacho ni KEN QRF 2 ni kikosi kilicho na askari wenye ujuzi na mafunzo ya juu sana. Hawa askari walichaguliwa moja kwa moja kutoka kikosi cha special forces ya Kenya kwa hiyo kuna mafunzo ya kufanya kazi katika eneo kama hili la mashariki mwa DRC kwa hiyo wanafanya operesheni wanafanya miradi mingine tofauti ambayo yote itachangia amani katika ili eneo. Sisi kama KEN QRF kuna jambo ambalo ningetaka kuangazia kwamba kwa wakati mwingi tunakwenda pale tunakuta mauaji yamefanyika na wale wahalifu. Sisi KEN QRF 2 ni kipaumbele chetu ni kwenda pale kabla uhalifu haujafanyika, kabla mauaji hayajafanyika. Tunaenda pale tunakaa hapo usiku nzima tunazuia na kuokoa maisha ya wale wakazi wa eneo hilo. Tangu tuje hapa hiyo ndio imekua kazi tunayoifanya sana. Tunashirikiana na wananchi wanatupa habari kwamba wale waasi ambao tunaita ADF wamepanga kuja kuvamia kijiji mahali fulani sisi tunachukua askari tukipewa kazi na brigedi yetu tunaenda huko na kuzuia waalifu kutekeleza mauaji"   

Akizungumzia pia miradi ya maendeleo wanayofanya walinda amani hao kutoka Kenya ili kusaidia wananchi wa DRC, "Hapa katika ili eneo kazi yetu kubwa ni operesheni ya kuleta amani ambayo tunafanya kwa ushikirikiano na jeshi la nchi hii, FARDC na pia tunashirikiana na polisi wa hapa. Lakini kuna miradi mingine pia  kandokando ambazo tunafanya zinazosaidia kuinua maisha ya wananchi kama kufungua barabara kutengeneza mahali ambako kuna shida, kujenga madaraja na pia tunafanya kitu ambacho kinaitwa medical camps ambapo tunaenda kutibu raia kulingana na uwezo tulionao".  

Je Luteni Kanali David Munoru ana wito gani kwa walinda amani wengine nchini humu DRC na pia kwa wakazi?  

"Walinda amani ningetaka kuwaomba kwamba tuendelee kuweka bidii zaidi kuzuia siyo kwenda wakati mauaji yamefanyika. Hpana. Tuweke bidii tuzuie mauaji tufanye operesheni ambayo imeongozwa na intelijensia ambayo tunaenda mahali tumesikia kwamba adui ADF wanafika sisi tunazuia na pia kwa raia kama tulivyokua na mkutano tarehe pili mwezi huu wa Mei wakati tulisema kwamba tuliwafundisha muweze kuleta habari kwa walinda amani. Wakazi waendelee kutupatia hiyo habari ili tuweze kuzuia mauaji badala mauaji yatimizwe na adui".  

Kwa upande wake Sajenti Magdaline Uhuru anatoa ujumbe wake kwa walinda amani wenzake na pia raia akisema, 

"Ujumbe wangu mkuu ningehimiza kontigenti wenzetu tuendelee kushirikiana pamoja kwa hudumisha amani DRC. Kama wakazi wa Eringeti tumejumuika nao pamoja kwakudumisha amani katika hilo eneo na matokeo yamekua mazuri hadi sasa. Toka Eringeti tumetembea sehemu za Ndalia Katabei na Maimoya nawezasema wakazi wametusaidia sana wamekua na na ushirikiano mkubwa na sisi".   

 

Mada hii kwa kina imeandaliwa na kuwasilishwa na George Musubao, DRC.