Zeid azungumzia elimu na ujauzito Tanzania

Picha:Msichana initiative
Mwanafunzi wa kike akiwezeshwa hatopata ujauzito shuleni.

Zeid azungumzia elimu na ujauzito Tanzania

Haki za binadamu

Haki za binadamu zinazidi kusiginwa maeneo mbalimbali duniani hata katika nchi ambazo kwa muda mrefu zimetambuliwa kuwa visiwa vya amani, asema Zeid Ra'ad Al Hussein hii leo katika ripoti yake kuhusu hali ya haki za binadadamu duniani.

Ukiukwaji mkubwa haki za binadamu umetapakaa duniani kote kuanzia kwenye migogoro, ubaguzi na hata kulikojulikana kuwa na amani ya muda mrefu hali ambayo inapaswa kukomeshwa mara moja.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Zeid Ra’ad al Hussein hii leo alipowasilisha ripoti yake ya mwaka ya hali ya binadamu duniani mbele ya Baraza la haki za binadamu mjini Geneva Uswisi.

Image
Wanafunzi darasani nchini Tanzania. Picha: UNICEF Video capture

Bara la Afrika likiongoza kwa kuwa na sehemu nyingi zenye machafuko ikiwemo Libya alikosema hakuna utawala wa sheria na ukwepaji wa sheria umekuwa ada hata kwa makosa makubwa kama mauaji na uhalifu dhidi ya ubinadamu kama vile kuwageuza watu watumwa.

Huko Tanzania ambako kwa miongo kadhaa kumejulikana kama kisima cha amani Zeid amesema haki za binadamu inaendelea kuzorota ikiwemo..

(Sauti Zeid Ra’ad Al Hussein)

 “Vikwazo vikali dhidi ya uhuru wa vyombo vya Habari na asasi za kiraia na ongezeko la idadi ya mashambulizi na kukamatwa kwa wanaoikosoa serikali.”

Image
Wanahabari wakiwa kazini. (Picha:UNESCO)

Ameongeza kuwa serikali  ya Tanzania pia imechukua msimamo mkali dhidi ya masuala muhimu ya jamii kama kuwakamata wanaharakati wa haki za watu wa mapenzi ya jinsia moja na waliobadili jinsia LGBTI, kuongezeka kwa mashambulizi jamii ya LGBTI na mashambulizi dhidi ya watu wanaotoa huduma ya afya ya uzazi. 

Kuhusu ukiukwaji wa haki ya elimu nchini humo amesema.

(Sauti Zeid Ra’ad Al Hussein)

“Sera ya kudumu ya serikali ya kuwanyima elimu zaidi wasichana waliopata ujauzito inashangaza, na nimesikitishwa na uamuzi wa mahakama kuu kuona sera hiyo siyo ya kibaguzi.”

Nako Burundi amesema ukiukwaji mkubwa wa haki unaendelea huku watu wakizidi kukwepa mkono wa sheria na hasa tangu kampeni ya serikali kuanza kutaka kubadilisha katiba.  Wanaharakati wa asasi za kiraia wamekuwa wakikamatwa na pia wanasiasa wa upinzani.

Image
Polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Kinshasa, DRC. (Picha:Unifeed video)

Kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hakusita kukemea kinachoendelea..

(Sauti Zeid Ra’ad Al Hussein)

Ninalaani kuendelea kwa ukiukwaji wa haki za msingi pamoja na kushambulia makanisa na maeneo ya kuabudu kunakofanywa na wanachama wa umoja wa vijana kwenye chama tawala. Serikali nayo haiweki mazingira ya kuwa na uchaguzi huru na wa kuaminika.”

Ingawa ameisifia Somalia kwa hatua iliyopiga ikiwemo kuanzishwa kwa tume ya kitaifa ya haki za binadamu, ameichagiza iimarishe taasisi zake na kurejesha amani nchini huo.

Kwa upande wa Kenya ameitaka serikali kuheshimu uhuru wa mahakama na kuichagiza kutekeleza maamuzi yanayotolewa na mahakama hizo na kusisitiza kuwa ni muhimu kwa Kenya kuhakikisha uwajibikaji kwa makosa ya ukiukaji wa haki za binadamu yaliyoripotiwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017 ikiwemo mauaji na ukatili wa kingono.