Muziki umenipatia ndugu ukimbizini-Eric Museveni

9 Oktoba 2019

Eric Museveni mwenye umri wa miaka 29, bila familia yake, alipoikimbia nchi yake ya Jamhuri ya kidemkorasia ya Congo mwaka 2015 na kuingia mjini Nairobi Kenya hakujua kuwa iko siku atapata familia mpya. Lakini Mungu si athumani, kupitia kipaji chake cha muziki, Eric amekutana na Peter Mulu kijana raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 30 ambaye amegeuka kuwa familia yake.

Eric na Peter walikutana katika shule ya muziki. Marafiki hawa wapya wanapenda kutengeneza muziki pamoja.

(Sauti ya Peter)

“Yeye ndiye nilikuwa namwona anakaa na watu vizuri. Mtu hana mambo mengi. Tulivyoonana na Museveni tukaanza kuongea akawa ananielezea mambo mengine najaribu kuelewa wengine walivyokuwa wananielezea kuhusu vita waliyoikimbia”

Kwa pamoja wameamzisha shule ya muziki na hivi sasa Eric na Peter wanaendesha mafunzo ya muziki kwa wakimbizi na wakenya. Eric anasimamia vipaji, huku Peter akisimamia upande wa noti za muziki na ala.

Eric anasema anaheshimu kila binadamu bila kujali hali,

(Sauti ya Eric)

“Uwe maskini au tajiri au ni nini. Tuna watu wanatoka Burundi, Rwanda, Congo na pia watu wa hapa, wakenya. Mimi nawachukulia kama marafiki zangu. Hatuwezi kusema hapa kuna wakenya hatuwezi kuimba. Muziki wenyewe ni lugha. Ilimradi kuna midundo mizuri.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud