Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya vituo vya raia Sudan ni kukiuka sheria za kimataifa: Nkweta-Salami

Katika Bandari ya Sudan, vifurushi vya dharura vya chakula vinagawiwa kwa watu wanaokimbia mapigano huko Khartoum.
© WFP/Mohamed Elamin
Katika Bandari ya Sudan, vifurushi vya dharura vya chakula vinagawiwa kwa watu wanaokimbia mapigano huko Khartoum.

Mashambulizi dhidi ya vituo vya raia Sudan ni kukiuka sheria za kimataifa: Nkweta-Salami

Amani na Usalama

Mratibu wa misaada ya Kibinadamu nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya kuendelea kwa ripoti za mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia huku mapigano ya kikatili yakiendelea kote Sudan.

Bi. Nkweta-Salami amesema "Nina wasiwasi mkubwa kwamba vifaa ambavyo ni muhimu kwa utendaji wa huduma za msingi ikiwa ni pamoja na maji, usafi wa mazingira, na huduma za afya, vinashambuliwa nchini Sudan," 

Mwezi huu wa Oktoba pekee kumekuwa na matukio kadhaa. Tarehe 9 Oktoba, makombora yalipiga hospitali ya Al Nao, mojawapo ya hospitali za mwisho zinazofanya kazi huko Omdurman, na kuua watu wawili na kujeruhi wengine watano wakati wafanyakazi wa matibabu walikuwa wakihudumia wagonjwa.

Makombora mengine manne yalilipuka karibu na hospitali hiyo na kusababisha vifo vya watu wengine wawili.

Mashambulizi 58 dhidi ya mfumo wa afya

Katika tarifa yake iliyotolewa mjini Port Sudan jana Jumatano Bi.Nkweta-Salami amesema “Haya ni mahsambulizi ya karibuni kabisa kwani tangu mwezi Aprili mwaka huu shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limethibitisha kuwepo kwa mashambulizi 58 katika mfumo wa afya na kusababisha vifo 31na watu 38 kujeruhiwa  ikiwa ni wastani wa mashambulizi 10 kwa mwezi.”

Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya vituo vya afya katika majimbo yaliyoathiriwa na mizozo havifanyi kazi, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za afya kwa mamilioni ya raia wasio na hatia.

Tarehe 21 Oktoba, mpango wa kusafisha maji wa Al Manara huko Omdurman ulishambuliwa na hivyo kusababisha kusitishwa kwa muda kwa usambazaji wa maji. 

Amesema “Aina hii ya usumbufu inatia wasiwasi sana kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea katika jimbo la Khartoum na maeneo mengine ya nchi. Zaidi ya hayo, mtambo wa maji ulioharibiwa sio tu kwamba unatatiza usambazaji wa maji kwa siku lakini pia unaweza kusababisha mgogoro wa muda mrefu unaoathiri kilimo, viwanda na maisha ya kila siku.”

Masjhambulizi lazima yakome kulinda raia

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, mara kwa mara nimetoa wito kwa vikosi vya wanajeshi vya Sudan, vikosi vya msaada wa haraka, na pande zote katika mzozo wa Sudan kulinda miundombinu ya kiraia. Amesema Bi. Nkweta-Salani na kusisitiza kuwa sheria za kimataifa ya kibinadamu ziko wazi katika suala hili. Pande zote kwenye vita lazima zichukue tahadhari mara kwa mara ili kuokoa vitu vya kiraia, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa kibinadamu na mali zao, na miundombinu muhimu. Mashambulizi haya lazima yakome.”

Mratibu huyo wa misaada ya kibinadamu ameongeza kuwa "Mgogoro huo umesababisha mateso yasiyoelezeka nchini Sudan kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo kabla. Heshima ya mwanadamu imetupwa nje ya dirisha, na kilichosalia ni kidogo tu, hata wodi za hospitali zimejaa watoto wagonjwa na waliojeruhiwa. Ninawasihi wahusika, tena kumalizia uchungu huu mbaya kwa kunyamazisha mtutu wa bunduki”.