Skip to main content

OCHA na wadau waendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha Ukraine  

Msafara wa Umoja wa Mataifa ukikaribia mstari wa mbele karibu na Chasiv Yar, katika eneo la Donetsk nchini Ukraine.
© UNOCHA
Msafara wa Umoja wa Mataifa ukikaribia mstari wa mbele karibu na Chasiv Yar, katika eneo la Donetsk nchini Ukraine.

OCHA na wadau waendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha Ukraine  

Msaada wa Kibinadamu

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura, OCHA Jens Laerke hii leo mjini Geneva Uswisi amesema wakati vita ikiendelea nchini Ukraine, ikiwa na athari mbaya kwa jamii hasa mashariki na kusini, OCHA na wadau wa kibinadamu wanaendelea kuwafikia watu wengi zaidi kwa msaada.  

Kufikia mwisho wa Aprili, OCHA ilikuwa imefikia watu milioni 5.4 mwaka huu, takribani watu 800,000 zaidi ya jumla ya idadi iliyosaidiwa mwishoni mwa Machi ambayo ni zaidi ya asilimia 60 ya waliofikiwa walikuwa wanawake na wasichana. 

Bwana Laerke ameeleza kuwa usaidizi unajumuisha pesa taslimu kwa zaidi ya watu milioni 2.1 na chakula kwa watu milioni 3.5, wakati karibu watu milioni tatu wamepata huduma za afya na dawa. Aina nyingine za usaidizi ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na bidhaa za usafi, makazi ya dharura, huduma za elimu kwa watoto na huduma za ulinzi, ikiwa ni pamoja na kuzuia ukatili wa kijinsia na msaada kwa walionusurika. 

Mamia ya mashirika ya kibinadamu yalihusika katika juhudi hii, wakifanya kazi na vikundi vya ndani na wanajamii wanaojitolea, ambao walichukua jukumu muhimu katika kupata usaidizi huo. Vita inayoongezeka imekuwa ikiathiri vibaya raia waliokuwa wakiishi karibu na mstari wa mbele wa vita ambao hawakuweza kurudi makwao, na watu kote nchini wanaoishi chini ya vitisho vya mashambulizi ya kila siku. 

"Vilipuzi pia ni tishio kwa wakulima wanaojaribu kurejea mashambani mwao na wasaidizi wa kibinadamu kutoa msaada. Hii ilihusu hasa katika mikoa ya kilimo ya Kharkiv, Mykolaiv na Kherson, ambapo ajali nyingi zinazohusiana na mabomu zinaripotiwa kila mwezi." Ameeza Msemaji huyo wa OCHA.  

Usaidizi kwa maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa kijeshi wa Urusi umebaki kuwa mdogo sana. Mwaka huu, kwa sababu ya hali mbaya ya usalama na mabadiliko katika mstari wa mbele, washirika wa kibinadamu wamepoteza ufikiaji wa karibu watu 60,000 katika miji na vijiji karibu 40 karibu na mstari wa mbele katika mikoa ya Donetsk, Kharkiv na Luhansk. 

Katika kujibu maswali ya wanahabari, Bw. Laerke amesema OCHA imetoa msaada na usaidizi wa pesa taslimu kwa karibu watu 60,000 katika maeneo yanayodhibitiwa na Shirikisho la Urusi.  

IFRC 

NKwa uoande wake Birgitte Bischoff Ebbesen, Mkurugenzi wa Kanda ya Ulaya wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC), amesema wiki hii imeadhimisha saa 11,000 tangu mzozo wa Ukraine ulipoongezeka. Zaidi ya mwaka mmoja baadaye, mamilioni ya watu bado wanaathiriwa moja kwa moja na vita, na mahitaji yanaongezeka na kubadilika. "IFRC inatoa wito kwa uwekezaji mpya ili kushughulikia mahitaji haya na hakuna wakati wa kurudi nyuma."  

Wengi ndani ya Ukraine wamekuwa wakikosa huduma za kimsingi kama vile maji, nishati na matibabu. Wengi hawakuweza kurudi majumbani mwao, kulipa kodi ya nyumba au kupata huduma za matibabu. Mamilioni ya watu walikuwa wakiishi nje ya nchi mahali ambapo huenda wasiweze kuzungumza lugha hiyo. Watu waliokimbia makazi yao ndani ya Ukraine wanakabiliwa na ukosefu wa mapato na kuongezeka kwa dhiki. IFRC imebainisha kuzorota kwa hali ya afya ya akili wakati wa shughuli za usaidizi wa kisaikolojia. Wale walio nje ya nchi wanahangaika kifedha, wengi wao wakiwa na madeni yanayoongezeka. Asilimia 41 ya watu wanaopokea usaidizi kutoka kwa IFRC wanategemea kuishi. Vizuizi vya lugha vinafanya iwe vigumu kupata kazi na kupata huduma za afya na elimu. Msaada wa kisaikolojia ni muhimu kwa watu hawa. 

IFRC imepanua operesheni yake ya usaidizi wa kibinadamu hadi angalau mwisho wa mwaka 2025 na imepanua ombi lake la dharura kuanzia Ukraine na nchi jirani hadi nchi 18 za bara la Ulaya. 

TAGS: Ukraine, OCHA, IFRC