Zaidi ya dola milioni 160 zahitajika kuokoa maisha ya mamilioni Ukraine 2019

1 Februari 2019

Umoja wa Mataifa na washirika wake wamasuala ya kibinadamu wamezindua ombi la dola milioni 162 ili kutoa msaada na kuwalinda watu milioni 2.3 walio katika hali mbaya Mashariki mwa Ukraine kwa mwaka huu wa 2019.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na mahitaji ya dharura , OCHA karibu watu milioni mbili wanahitaji msaada ama wako katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali Ukraine au ndani ya kilometa 20 kutoka mstari unaoligawanya eneo hilo la Mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis , msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema vita nchini humo vinaendelea kuathiri maisha ya raia hususan kwa magruneti na risasi kutoka kwa walenga shabaha kila siku hasa kwa watu wanaoishi karibu na mstari huo unaoligawa eneo la Mashariki mwa Ukraine na kuongeza kwamba

(SAUTI YA JENS LAERKE)

“Watu Zaidi ya 3300 wameuawa na wengine takribani 9000 kujeruhiwa tangu machafuko yaanze 2014. Pia machafuko hayo yameharibu na kusambaratisha nyumba, hospitali, shule, barabara, mifumo ya kusambaza maji na miundombinu mingine ya raia na hivyo kuvuruga au kukata fursa za wananchi kupata huduma muhimu kama za tiba.”

Amesema sehemu kubwa ya makazi ya raia hususan kwenye maeneo yanayodhibitiwa na wapinzani yana mabomu ya kutegwa ardhini na vifaa vingine vya mlipuko vya kivita ambapo mwaka 2018 majeruhi na vifo 2070 vilitokana na mabomu na vilipuzi hivyo.

OCHA inasema fedha zitakazopatikana kutokana na ombi hilo zitatumiwa na mashirika 43 ya Umoja wa Mataifa na kimataifa katika kutekeleza utoaji wa misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, malazi, vifaa vya nyumbani, msaada kwa ajili ya msimu wa baridi, maji safi, elimu na huduma bora za afya kwa watu wanaoziihitaji.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter