Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na wadau wa misaada ya kibinadamu wanasaidia watu 150,000 Kharkivska Ukraine

Misaada ya dharura imeanza kufika kwenye maeneo ambayo hivi karibuni yameanza kufikiwa na mashirika ya kibinadamu kwenye eneo la Kharkivska oblast, Ukraine.
© WFP
Misaada ya dharura imeanza kufika kwenye maeneo ambayo hivi karibuni yameanza kufikiwa na mashirika ya kibinadamu kwenye eneo la Kharkivska oblast, Ukraine.

UN na wadau wa misaada ya kibinadamu wanasaidia watu 150,000 Kharkivska Ukraine

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA limesema wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wameanza kusafirisha misaada ya kuokoa maisha siku chache tu baada ya serikali ya Ukraine kutangaza kuwa imechukua tena udhibiti wa eneo la Kharkivska Oblast.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo jumuiya ya misaada ya kibinadamu, kwa muda wa siku 10 zilizopita, imetuma sehemu ya kwanza ya msafara uliosheheni misaada ya dharura katika maeneo ya mkoa wa Kharkivska ambayo hivi karibuni yamefikiwa na mashirika ya misaada.

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa OCHA nchini Ukraine Denise Brown amesema “Nilitembelea baadhi ya maeneo haya wiki jana, ikiwa ni pamoja na Balakliia, na nilijionea mwenyewe uharibifu na kiwewe kilichosababishwa na vita kwa watu wa maeneo hayo. Katika baadhi ya maeneo, tumeona nyumba, vituo vya afya na shule zikiwa zimeharibiwa au kusambaratishwa. Mamlaka inafanya kila iwezalo kurekebisha uharibifu wa mifumo ya gesi na nishati ya umeme, lakini maelfu bado hawana usambazaji wa huduma hizo muhimu. Na kuhakikisha watu wanasaidiwa kuwa na mahali pa joto na salama pa kukaa sasa kwa vile msimu wa baridi umewadia ni suala la uhai au kifo kwa maelfu ya watu.”

OCHA inasema zaidi ya watu 73,000 karibu nusu ya wakazi wanaoishi katika maeneo hayo tayari wamepokea chakula na vifaa vya usafi 12,000 vimesambazwa pamoja na vifaa vya nyumbani, ikiwa ni pamoja na svyombo vya jikoni, taa za zinazotumia nishati ya jua au sola, na mablanketi kwa watu 15,000. 

Pia dawa, vifaa vya matibabu ya upasuaji na dharura, vya kutosha kutibu watu 10,000 katika wiki zijazo, vimesambazwa katika vituo vya afya katika maeneo yote na upelekaji wa vitu vingine muhimu utaendelea.

Denis Brown amesema jumuiya ya misaada ya kibinadamu inafanya kazi kwa karibu na mamlaka za kitaifa na za mitaa, pamoja na vikundi vya kujitolea, kutoa misaada na kusaidia watu ambao wamevumilia hali ya kutisha ya miezi saba ya vita. 

Ameongeza kuwa "Utoaji wa misaada ya kibinadamu ni muhimu kwa mahitaji ya dharura ikiwemo, kutibu waliokumbwa na kiwewe na hofu kubwa ya kwamba vita vitachukua muda mrefu zaidi. "