Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kapteni Cecilia Erzuah ashinda tuzo ya Mchechemuzi wa masuala ya kijinsia kwenye operesheni za UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kushoto) akimkabidhi Tuzo ya Mtetezi Bora wa Kijeshi wa Jinsia kwa 2022 Kapteni Cecilia Erzuah kutoka Ghana ambaye alihudumu katika Kikosi cha Usalama cha Muda cha Umoja wa Mataifa cha Abyei (UNISFA).
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kushoto) akimkabidhi Tuzo ya Mtetezi Bora wa Kijeshi wa Jinsia kwa 2022 Kapteni Cecilia Erzuah kutoka Ghana ambaye alihudumu katika Kikosi cha Usalama cha Muda cha Umoja wa Mataifa cha Abyei (UNISFA).

Kapteni Cecilia Erzuah ashinda tuzo ya Mchechemuzi wa masuala ya kijinsia kwenye operesheni za UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres amemtangaza Kapteni Cecilia Erzuah kutoka Ghana kuwa mshindi wa tuzo ya kila mwaka ya Mchechemuzi wa Masuala ya jinsia kwenye operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa.

Akihutubia katika maadhimisho ya siku ya walinda amani duniani yaliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Bwana Guterres amesema Kapteni Erzuah ameibuka kidedea kutokana na mchango wake kama mlinda amani wa kijeshi kwenye ujumbe wa mpito wa Umoja wa Mataifa huko Abyei nchini Sudan Kusini.

Eneo la Abyei lilikuwa ni uwanja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambako baada ya kuona madhila yanayokumba jamii hususan wanawake kwenye mizozo alishiriki kikamilifu katika kuchagiza kuona wanawake wanajumuishwa na wanashiriki kwa dhati kwenye michakato ya amani.

“Ninajivunia kumkabidhi Kapteni Erzuah tuzo ya mchechemuzi bora wa mwaka wa masuala ya kijinsia ya Kijeshi kwa kazi yake huko Abyei kama Kamanda wa Kikosi cha Ushirikiano cha Ghana tangu Machi 2022.”

Guterres amewashukuru Kapteni Erzuah na wanawake wote walinda amani kwa huduma na uongozi wao.

Kapteni Erzuah alifanya nini?

Akiwa kamanda wa kikosi huko Abyei, alijionea athari kubwa ya vita kwenye jamii nzima hususana kwa wanawake na alijitahidi kuhakikisha kuwa sauti zao zinasikika na kuwakilishwa.

Kazi kuu ya kikosi alichokiongoza ilikuwa ni ktembelea jamii za wenyeji ili kusikia matatizo yao, kueleza kazi ya walinda amani, na kujenga uaminifu.

Ushirikiano wake na uongozi wa mtaa, vikundi vya wanawake na vijana umekuwa muhimu kwa mafanikio ya misheni.

Pia aliandaa mijadala kuhusu unyanyasaji wa majumbani na usawa wa kijinsia, ambayo ilisababisha wanawake wa eneo hilo kujiandikisha katika kamati za ulinzi wa jamii ambazo hutoa taarifa za mapema zinazo ijulisha jamii iwapo kuna vitisho vya usalama katika maeneo yao.

Katika kila nyanja, kazi ya Kapteni Erzuah imekuwa ikitumika kuweka viwango vya kuhakikisha mahitaji na changamoto za wanawake zinaakisiwa katika shughuli zote za kulinda amani.

Akipokea tuzo hiyo Kapteni Erzuah ameshukuru kwa kutangazwa mshindi na kupokea tuzo hiyo. “Tuzo hii inasisitiza juhudi na kujitolea kwa kikosi changu kuelekea usawa wa kijinsia na ushirikishwaji, huku nikitimiza Majukumu ya Kikosi cha Usalama cha Muda cha Umoja wa Mataifa huko Abyei.”

Mshindi huyo ameeleza pia umuhimu wa kuhakikisha kuna usawa wa kijinsia na kutoa wito wa kila nchi kuhakikisha wanatuma wanajeshi na askari wanawake katika ulinzi wa amani kwani umuhimu wao ni kiwango cha juu.

Kila nchi itathmini haja ya kuongeza wanawake kwenye michakato ya amani

Katibu Mkuu Guterres kabla ya kumkabidhi tuzo Kapteni Cecilia Erzuah aligusia azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalohusu Wanawake, Amani na Usalama na kusema mi moja ya  mafikio makubwa zaidi ambayo Baraza hilo limewahi kupitisha.

Amesema azimio hilo muhimu linakumbusha kuwa hawawezi kuwa na amani ya kudumu bila kuwashirikisha wanawake katika kila hatua.

“Lakini hata leo, timu nyingi za mazungumzo na michakato ya amani hutawaliwa kabisa na wanaume. Amesema Mkuu huyo wa UN na kueleza kuwa “ni juu yetu sote - serikali, jamii na maafisa wa serikali - kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamillifu, ikiwa ni pamoja na kama viongozi, katika kujenga na kudumisha amani.”

Amehitisha kwa kusema azimio nambari 1325 linatukumbusha kwamba walinda amani wetu wanawake sio tu kwamba wanaunga mkono amani na usalama wa kimataifa lakini pia wanaongoza njia.