Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake Sudan Kusini washukuru kuwepo kwa vituo salama vilivyoanzishwa na UN

Aweil kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini ambako kituo hiki ambapo wanawake wanakusanyika kubadilishana taarifa kuhusu waliyowakumba hususan maswala ya ukatili wakijinsia.
UN Photo/Isaac Billy
Aweil kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini ambako kituo hiki ambapo wanawake wanakusanyika kubadilishana taarifa kuhusu waliyowakumba hususan maswala ya ukatili wakijinsia.

Wanawake Sudan Kusini washukuru kuwepo kwa vituo salama vilivyoanzishwa na UN

Amani na Usalama

Vituo salama vilivyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuepusha wanawake na wasichana dhidi ya ukatili wa kijinsia nchini Sudan Kusini vimekuwa muarobaini na mwokozi kwa makundi hayo.

Miongoni mwa vituo hivyo ni kile kilichopo El Ghazal ambacho hivi karibuni kilitembelewa na Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer.

Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa  Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS alitembelea kituo hicho kilichopo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ambacho kimekuwa makazi mengine ya wanawake hao ambapo hukutana hapa kubadilishana taarifa na uzoefu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, jinsi ya kuzuia vitendo hivyo na wanafurahi kuwa na kituo hicho.

Zaidi ya hayo, wanawake hawa pia wanalitumia eneo hili kama kituo cha kujifunzia ambapo wanapata ujuzi wa aina mbalimbali ili kuboresha ustawi wao, mathalani wanatengeneza shanga ambazo zina gharama kati ya dola 10 hadi 15, kiasi kikubwa katika nchi yenye viwango vya chini vya mapato.

Na wakati ambapo wanakuwa hawatengenezi vitu, wanafurahi kwa kuimba na kucheza, ambayo ni tiba kwa kiwewe walichopata kutokana na majanga waliyopitia. Mwanamke huyu ni mnufaika wa kituo hicho

(Mnufaika wa kituo salama)

“Magumu yote tuliyokuwa tunakabiliana nayo kama wanawake, yamepungua na tunakuja hapa kutatua matatizo yetu. Wakati tunaporudi nyumbani yanakuwa wamekwisha.Ndiyo maana mara zote tunakuja kutitumia siku yetu hapa. Kituo hiki kimetsaidia sana sisi wanawake.”

Kitengo cha usaidizi na ulinzi cha UNMISS kinafanya kazi na wadau wengine kujenga vituo kama hivyo vya usalama kwa ajili ya wanawake ambapo David Shearer amesema angependa kuona ni kwa namna gani Umoja wa Mataifa unaweza kushirikiana na serikali katika eneo hilo kutengeneza fursa zaidi kwa watu na hususani wanawake.

(Sauti ya David Shearer)

“Nimefurahi sana kuwa hapa na wanawake katika kituo hiki cha wanawake kwasababu kwa Umoja wa Mataifa na kwa watu wengi kutoka Umoja wa Mataifa ambao wako nami hapa, mstakabali wa wanawake ni muhimu sana kwetu nchini Sudan Kusini.”

Vituo salama kwa ajili ya wanawake na wasichana  vilianzishwa na Umoja wa Mataifa kwa kushauriana na jamii, na wanawake na wasichana kushirikishwa katika kuichora ramani ya jamii yao na kuonesha ni nyakati gani na wapi ni salama na ambazo si salama.