Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mipango ya kupunguza ukubwa wa operesheni isiathiri idadi ya wanawake walinda amani- Guterres

Moja ya vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
UN/Eskinder Debebe
Moja ya vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Mipango ya kupunguza ukubwa wa operesheni isiathiri idadi ya wanawake walinda amani- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakati huu ambapo mipango ya kupunguza watendaji kwenye operesheni za ulinzi wa amani unaendelea ni vyema kuwa makini kuzingatia idadi ya wanawake walinda amani.

Guterres amesema hayo leo jijini New York, Marekani wakati akihutubia mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifakuhusu wanawake na ulinzi wa amani katika muktadha wa kuimarisha amani na usalama duniani.

Amesema idadi kubwa ya wanawake kwenye operesheni za ulinzi wa amani imedhihirisha kuwa ni muhimu katika kufanikisha jukumu la ulinzi wa raia na zaidi ya yote hujenga imani ya wanajamii kwa walinda amani.

Ushahidi unaonyesha kuwa kuwepo kwa idai kubwa ya walinda amani wanawake kunafanya operesheni za ulinzi wa raia kuwa halali zaidi na zinakidhi mahitaji ya jamii za wenyeji,” amesema Guterres akisema wanawake walinda amani walio kwenye doria wako katika nafasi nzuri zaidi kuwafikia wanawake na wanaume wanaokabiliwa na changamoto ikiwemo kuripoti zaidi vitendo vya ukatili wa kingono na pia kupungua kwa vitendo hivyo.

Kwa mantiki hiyo amesema tayari wamewasilisha pendekezo katika kamati ya tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na bajeti ili kuhakikisha kuwa idadi hiyo inazingatia mkakati wa usawa wa jinsia kwenye operesheni za ulinzi wa amani ulioanza kutekelezwa mwaka huu.

Bwana Guterres pia akazungumzia suala la kuongeza idadi ya walinda amani wanawake akisema suala lisiwe idadi bali pia ufanisi akisema sasa inahitajika zaidi maofisa wa magereza na wale wa kusimamia haki.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

“Hili ndio eneo lenye changamoto zaidi hivyo tuna maombi ili tuweze kushughulikia changamoto hizi , mosi kwa kuteua wanawake maofisa na pili kwa kujikita kwa wanawake wanajeshi na polisi,” amesema Katibu Mkuu.

Akihutubia mkutano huo, Meja Jenerali Kristin Lund ambaye ni mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kusimamia sitisho la mapigano huko Mashariki ya Kati, UNTSO pamoja na kuelezea uzoefu wake akiwa mwanamke mlinzi wa amani na mkuu wa operesheni hiyo katika kusongesha ushiriki wa wanawake kwenye ulinzi wa amani amebadili fikra potofu.

“Mfano tu, kwenye chumba cha mazoezi, kambi zote zina vyumba vya mazoezi na takribani katika vyumba vyote hivyo kuna mabandiko ya picha ukutani yakiwa na picha za wanawake walio nusu uchi. Ni wanawake wangapi wanakwenda kwenye mazoezi wakiwa nusu uchi?” amehoji Meja Jenerali Lund.

Amesema badala yake kuta za vyumba hivyo vya mazoezi vinapaswa kuwa na mabandiko ya picha za watu wakionyesha jinsi ya kufanya mazoezi na mavazi ya kawaida.

Meja Jenerali Lund amesema tayari huko Cyprus kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa mabandiko yote ya picha za wanawake nusu uchi zimeondolewa na mtazamo wa fikra umebadilika sambamba na kuhakikisha kuwa timu za michezo zinajumuisha wanawake na wanaume.

Kutoka Sudan Kusini, Loma Merekaje, Katibu Mkuu wa shirika la kiraia la kufuatilia mipango na pia mwakilishi wa wanawake kwenye kamati ya kitaifa ya marekebisho ya katiba ameunga mkono hoja ya uwepo wa wanawake walinda amani.

Amesema uwepo wa wanawake hao umefanya mazingira kuwa shwari na wananchi wanaweza kuendelea na shughuli zao.

Hata hivyo ametaka Umoja wa Mataifa uhakikishe kuwa harakati zozote zinazopangwa kufanyika nchini Sudan Kusini zishirikishe wadau wa nchi husika.