Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake 80 ni miongoni mwa  polisi 160 kutoka Rwanda waliowasili UNMISS : 

Kellen Busingye wa UNPOL, kutoka Rwanda-(Picha:UNMISS/Eric Kanalstein)

Wanawake 80 ni miongoni mwa  polisi 160 kutoka Rwanda waliowasili UNMISS : 

Amani na Usalama

Kikosi kipya cha maafisa wa polisi kutoka Rwanda kikiwa na wanawake 80 na wanaume 80 kimewasili nchini Sudan Kusini kujiunga na mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo UNMISS.

Hapa ni Juba mji mkuu wa Sudan kusini maafisa wa polisi 160 wanawake na wanaume wakiwa wamevalia sare zao ndio kwanza wamewasili kutoka Rwanda kuja kuanza majukumu mapya kwenye mpango wa UNMISS.

Majukumu hayo yatakayojumuisha kudhibiti mkusanyiko mkubwa wa watu, kusaidia ufikishaji wa misaada ya kibinadamu na ulinzi wa majengo na ofisi za Umoja wa Mataifa.

Teddy Ruyenzi ni kamanda wa kikosi cha polisi wa Rwanda walioko Juba ana uzoefu mkubwa katika operesheni za ulinzi wa amani kuanzia Haiti, Mali na sasa Sudan kusini, anasema idadi kubwa ya wanawale waliowasili ni hamasa kwa wengine

 

(SAUTI YA TEDDY RUYENZI)

“Itakuwa ni kitu kizuri kwa wanawake  wa jamii ya Sudan kusini lakini pia duniani kote kwa sababu watajua kwamba wanawake wakiwezesha wanaweza kufanya chochote kama walivyo wanaume."

 

Akiunga mkono kuwa na idadi kubwa ya wanawake polisi kwenye operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, inspekta Speciose Dusabe anafunguka

 

(SAUTI YA INSPEKTA SPECIOSE DUSABE)

Watoto na wanawake kwa kawaida ndio makundi yanayoathirika zaidi na vita na kunapokuja suala la ukatili na unyanyasaji wa kijinsia inakuwa rahisi kuwa wazi zaidi na kwa  kutoa tarifa zao kwa polisi wanawake kuliko wanaume.

 

Inspekta Dusabe na wenziwe wamechaguliwa na jeshi la polisi la Rwanda kwa sababu ya uzoefu na ujuzi wao, lakini pia wamepatiwa mafunzo ya miezi sita na kufaulu mitihani kadhaa kabla ya kutia mguu Juba ambako kutakuwa maskani ya kikosi chao kipya.