Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Malawi hatarini kukumbwa na utapiamlo, Umoja wa Mataifa wachukua hatua.

Uji wenye lishe bora kwa watoto walioathiriwa na kimbunga Freddy. Watoto walionufaika na mlo huu wako Mayela mjini Blantyre kusini mwa Malawi.
UNICEF/Thoko Chikondi
Uji wenye lishe bora kwa watoto walioathiriwa na kimbunga Freddy. Watoto walionufaika na mlo huu wako Mayela mjini Blantyre kusini mwa Malawi.

Watoto Malawi hatarini kukumbwa na utapiamlo, Umoja wa Mataifa wachukua hatua.

Msaada wa Kibinadamu

Takribani watoto 573,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini Malawi wako hatarini kukumbwa na utapiamlo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto duniani,  UNICEF huku likisema linahitaji dola milioni 87.7 kukidhi mahitaji ya watu milioni 6.5 wakiwemo watoto milioni 3.3 nchini humo, ikiwa ni ombi jipya la fedha lililotolewa leo.

UNICEF kupitia taarifa yake iliyotolewa jijiini Lilongwe Malawi hii leo, inasema maendeleo yaliyopatikana hivi karibuni ya kukabili utapiamlo yanayoyoma kutokana na uhaba mkubwa wa chakula ukigubikwa na matukio ya mara kwa mara ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa yanayozuilika, ukosefu wa utulivu wa kiuchumi na ukosefu mkubwa wa ufadhili kwenye sekta za kijamii.

Taarifa hiyo inasema Malawi bado inazingirwa na kiza kinene cha athari mbaya za kimbunga Fredy kilichokumba taifa hilo mwezi Machi na kuacha hadi leo hii watu 659,000 wakimbizi wa ndani wakiwemo watoto.

Halikadhalika mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu bado unaendelea na tayari umesababisha vifo vya watu 1,759.

Dalitso Dines mwenye umri wa miaka 14 in mwanafunzi wa darasa la 8 na manusura wa kimbunga Freddy. Hapa yuko darasani kwenye shule ya msingi ya Chumani huko Mulanje kusini mwa Malawi akijisomea. Hii ni tarehe 23 Machi 2023.
UNICEF/Thoko Chikondi
Dalitso Dines mwenye umri wa miaka 14 in mwanafunzi wa darasa la 8 na manusura wa kimbunga Freddy. Hapa yuko darasani kwenye shule ya msingi ya Chumani huko Mulanje kusini mwa Malawi akijisomea. Hii ni tarehe 23 Machi 2023.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Malawi Gianfranco Rotigliano anasema watoto nchini Malawi wanakabiliwa na mlolongo wa majanga. Ukosefu wa uhakika wa kupata chakula ukichochewa na janga la mabadiliko ya tabianchi, mlipuko wa magonjwa na kutwama kwa uchumi duniani, vyote vinatishia maisha ya mamilioni ya watoto.

Amerejelea ombi la Hatua za Kiutu kwa Watoto, HAC lililozinduliwa leo na UNICEF likionesha ongezeko la matukio ya utapiamlo miongoni mwa watoto katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo mwaka 2023 pekee watoto 62,000 wenye umri wa kati ya miezi 6 hadi miaka 5 wako hatarini kukumbwa na unyafuzi au udumavu.

Ni kwa mantiki hiyo UNICEF imeongeza ombi lake kwa usaidizi Malawi kutoka zaidi ya dola milioni 52 hadi dola milioni 87 ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 6.5 wakiwemo watoto milioni 3.3.

Fedha hizo zitatumika kununua mahitaji ya vyakula vilivyo tayari kuliwa ili kutibu unyafuzi, kupata huduma za maji safi na salama, huduma za kujisafi, afya, lishe, elimu, ulinzi dhidi ya watoto na miradi ya fedha taslimu.

Bwana Rotigliano amesema bila usaidizi wa kifedha, kaya maskini na za Watoto walio hatarini watasalia bila huduma za msingi na zaidi ya yote amesema pamoja na misaada hiyo ni lazima kujengea mnepo ili kupunguza madhara makubwa ya milipuko na dharura za kiutu.