Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiliniki za UNICEF 'zinazotembea' msaada kwa waathirika wa kimbunga Freddy nchini Malawi

Mtoto wa miezi sita anapimwa malaria baada ya kimbunga Freddy kusababisha mafuriko na uharibifu nchini Malawi.
© UNICEF/Thoko Chikondi
Mtoto wa miezi sita anapimwa malaria baada ya kimbunga Freddy kusababisha mafuriko na uharibifu nchini Malawi.

Kiliniki za UNICEF 'zinazotembea' msaada kwa waathirika wa kimbunga Freddy nchini Malawi

Afya

Wananchi wa Malawi walioathirika na Kimbunga Freddy wamepongeza mbinu ya kutumia kilniki za kuhama kwa njia ya magari iliyotumiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kuwahudumia wanawake na watoto nchini Malawi baada ya kimbunga Freddy kilicholipiga eneo hilo takribani miezi mwili iliyopita. Anold Kayanda na maelezo zaidi. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) linasema kimbunga Freddy kilichotokea kati ya Februari 5 na Machi 14 kiliwaacha watoto wa Malawi milioni 2.9 hatarini na katika uhitaji mkubwa wa msaada wa kibinadamu. 

Na katika msingi huo bado UNICEF inawaomba wahisani duniani kote kuichangia dola za Marekani milioni 52.4 kupitia ombi la Hatua ya Kibinadamu kwa ajili ya kufanikisha kutoa msaada wa kuokoa maisha ya watoto na wanawake nchini Malawi, ikiwa ni pamoja na wale walioathiriwa na Kimbunga Freddy hicho.  

Hata hivyo UNICEF katika hali hiyo hiyo ya uhaba wa ufadhili bado ilifanikiwa kutoa msaada kwa watu walioalazimika kuishi kwenye makambi baada ya kimbunga hicho. Mary Kwatani ni mmoja wao, “Nilikuja kambini kwa sababu nilipoteza nyumba yangu kutokana na mafuriko. Nilikuja hapa kutafuta makazi kwa sababu afya ya watoto wangu ilikuwa mbaya kutokana na lishe duni.” 

Kwa haraka UNICEF ilichukua hatua ikaleta kiliniki za kwenye magari ili kuleta huduma tiba kwa ajili ya, wajawazito na wanaonyesha na watoto chini ya umri wa miaka mitano. 

Mary Kwatani ni mnufaika anasema, "Kiliniki hizi zinazotembea zimekuwa msaada kwangu kwa sababu nilikuwa nasafiri umbali mrefu kufika hospitalini lakini sasa wahudumu wa afya wanaweza kutufikia kupitia kiliniki zinazohama." 

Kimbunga Freddy ambacho kilizipiga nchi kadhaa kusini mwa Afrika, kwa Malawi kiliathiri moja kwa moja wilaya 15 zilizopo kusini mwa nchi ya Malawi na kuathiri maisha ya watu na makazi.