Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HRC lamulika ukiukwaji wa haki za binadamu Sudan

Takriban watu milioni 2 hadi milioni 2.5 wanatarajiwa kutumbukia kwenye janga la njaa nchini Sudan
© WFP/Peter Louis
Takriban watu milioni 2 hadi milioni 2.5 wanatarajiwa kutumbukia kwenye janga la njaa nchini Sudan

HRC lamulika ukiukwaji wa haki za binadamu Sudan

Haki za binadamu

Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za binadamu leo limefanya kikao maalum kushughulikia athari za vita inayoendelea nchini Sudan kwa haki za binadamu. Katika taarifa yake kwenye kikao hicho Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema mapigano hayo "yanaitumbukiza nchi hiyo yenye mateso mengi katika janga kubwa".

Tangu tarehe 15 Aprili, takriban raia 487 wameuawa, hasa katika miji ya Khartoum, El Geneina, Nyala na El Obeid huku takwimu halisi zikisemekana kuwa ni za juu zaidi, zaidi ya watu 154,000 wamelazimika kuikimbia nchi hiyo, na inakadiriwa watu wengine zaidi ya 700,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani mipaka ya Sudan.

Ameongeza kuwa na wale ambao wamesalia katika maeneo yaliyoathiriwa na mzozo wako kwenye hatari kubwa.

Kutoka nuru ya tumaini hadi janga la kibinadamu

Bwana Türk amelikumbusha Baraza hilo kwamba mwaka wa 2019 Sudan ilionekana kama mnara wa matumaini baada ya maandamano maarufu yaliyoongozwa na wanawake na vijana na kuupindua udikteta au utawala wa kiimla wa Omar al-Bashir uliodumu kwa miongo mitatu.

Pia amezungumza kuhusu ziara yake nchini humo miezi sita iliyopita jukumu lake la kwanza kama mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa wakati kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia kilikuwa karibu.

Akikumbuka mikutano yake ya wakati huo na majenerali wote wawili hasimu, mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa ujumbe wake umekuwa kusisitiza uwajibikaji na haki za binadamu kama nguzo muhimu kwa makubaliano yoyote yajayo.

"Leo, uharibifu mkubwa umefanywa, na kusambaratisha matumaini na haki za mamilioni ya watu," ameongeza bwana Türk.

Mashambulizi katika maeneo ya raia

Kamishina mkuu amesema mjini Khartoum, mapigano kati ya vikosi hivyo viwili vya wanajeshi wa jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF)  vilivyojihami, makombora na mashambulizi ya anga yamefanyika katika maeneo ya makazi yenye watu wengi, na mamilioni ya watu sasa wanahaha kupata chakula, mafuta na fedha.

Katika baadhi ya maeneo ya Darfur, pamoja na maeneo ya Blue Nile na Kordofan, ghasia kati ya makundi ya kijeshi zimesababisha mapigano baina ya makabila. Huko Darfur Magharibi, takriban watu 100 wameuawa, na maelfu kuyakimbia makazi yao, kutokana na ghasia kati ya jumuiya zinazojiita "Waarabu" na vikundi vya Masalit, vinavyoshirikiana na Vikosi vya RSF kwa upande mmoja na vikosi vya SAF kwa upande mwingine.

Kamishina mkuu amelaani vikali "unyanyasaji huu mbaya, ambapo pande zote mbili zimekiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu, haswa kanuni za kutofautisha raia na wapiganaji na tahadhari".

Volker Türk ameyataka mataifa yote yenye ushawishi katika kanda hiyo kuzichagiza pande hasimu katika mzozo kwa kila njia ili kupata suluhu ya mzozo huo.

Ni lazima kulinda taifa letu: Sudan

Kwa upande wake Hassan Hamid Hassan, mwakilishi wa kudumu wa Sudan katika ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, amesema kinachofanyika ni mambo ya ndani, na kinachofanywa na jeshi la Sudan ni wajibu wa kikatiba kwa majeshi yote ya dunia.

Msimamo wa Sudan katika kikao hicho maalum umejikita katika mambo yafuatayo,  huku ikirejelea kipaumbele cha serikali katika kukuza na kulinda haki za binadamu, chini ya hali mbaya ya sasa mapigano ya kijeshi na vifo vya waathirika, ilikuwa ndio kipaumbele, ambacho ni kufikia usitishaji vita na kuokoa maisha, kulingana na azimio la kimataifa la Haki za binadamu.

Kuhusu Baraza Kuu: HRC

Hii sio mara ya kwanza kikao maalum kuhusu Sudan kufanyika kwenye Baraza la haki za binadamu, kikao cha mwisho kuhusu Sudan kilifanyika tarehe 5 Novemba 2021.

Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilianzishwa mwaka 2005, kuchukua nafasi ya Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Baraza la Haki za binadamu ni chombo cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na linakutana mara kwa mara, angalau mara tatu kwa mwaka.

Moja ya vikao hivyo ni Baraza Kuu na huchukua wiki kumi.

Baraza linaweza kufanya vikao maalum vya dharura kwa ombi la theluthi moja ya wanachama wake, ikiwa ni pamoja na kushughulikia hali za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika nchi moja moja.

Jumla ya vikao 36 vya aina hiyo vimefanyika tangu 2005. Vikao vitatu vya mwisho vilihusu hali ya Iran (2022), Ukraine (2022), Ethiopia (2021).

Baraza hilo linajumisha nchi 47. Kundi la mataifa ya Ulaya Mashariki lina viti 6 katika Baraza hili.

Asia na Afrika zina viti 13 kila moja, Amerika ya Kusini ina viti 8 na kundi la mataifa ya Ulaya Magharibi, Marekani, Canada na Israel lina viti 7.

Wajumbe wa Baraza huchaguliwa kwa miaka mitatu kwa kura nyingi za wajumbe wa Baraza Kuu kwa kura ya siri ya moja kwa moja.