Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kutisha ya zaidi ya watu milioni 10 waliokimbia makazi yao kutokana na mizozo nchini Sudan isipuuzwe - IOM

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope, (mwenye skafu ya buluu) akizungumza na wanawake wa Somalia wakati wa ziara yake ya siku  nne nchini humo.
IOM
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope, (mwenye skafu ya buluu) akizungumza na wanawake wa Somalia wakati wa ziara yake ya siku nne nchini humo.

Hali ya kutisha ya zaidi ya watu milioni 10 waliokimbia makazi yao kutokana na mizozo nchini Sudan isipuuzwe - IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM Amy Pope amesema hali ya kutisha inayokumba zaidi ya watu milioni 10 waliofurushwa kwenye makazi  yao nchini Sudan kutokana na mapigano haipaswi kupuuzwa. Taarifa ya IOM iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na Port Sudan nchini Sudan imemnukuu akieleza kwamba watu milioni 10.7 sasa wamekimbia makazi yao kutokana na migogoro nchini Sudan, na kati yao hao, milioni tisa wamo  ndani ya nchi hiyo kulingana na takwimu mpya kutoka IOM. 

Shirika hilo linatoa wito wa juhudi za pamoja za jamii ya kimataifa ili kuongeza haraka mwitikio wa usaidizi wa kibinadamu kwa wakimbizi hao ambao idadi yao ni kubwa zaidi ikilinganishwa na kwingineko kwenye wakimbizi wa ndani duniani. 

Bi. Pope ameendelea kusema wasudan wengine milioni milioni 1.7 wamekimbia ghasia hizo na kuelekea katika nchi jirani, idadi kubwa saw ana asilimia 62 wakiwa ni raia wa Sudan. 

Wanawake na wasichana wakichota maji kwa ajili ya familia zao katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan.
© UNICEF/Adriana Zehbrauskas
Wanawake na wasichana wakichota maji kwa ajili ya familia zao katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan.

Mkimbizi wa ndani 1 kati ya 8 yuko Sudan 

Idadi kubwa ya waliokimbia Sudan wamesaka hifadhi Chad ikiwa in asilimia 37, huku Sudan Kusini ikiwa na asilimia 30 na Misri ikiwa na asilimia 24. Ethiopia, Libya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ikiwa imehifadhi wasudan wengine lakini kwa kiwango kidogo. 

Kulingana na Bi. Pope, "hadi leo, mkimbizi mmoja kati ya kila wakimbizi wanane wa ndani duniani yuko nchini Sudan. Mahitaji yao ni makubwa: uhaba mkubwa wa chakula, malazi, huduma za afya, na usafi wa mazingira, yote yanachangia kuwaweka katika hatari kubwa ya magonjwa, utapiamlo, na vurugu. Hata hivyo mwitikio wa kibinadamu hadi sasa hautoshi kukidhi mahitaji makubwa. Hatuwezi kuwapa kisogo mamilioni ya watu wanaohitaji msaada.”

Miezi 9 iliyopita wasudan milioni 6 wamefurushwa 

Hali kadhalika, Mkuu huyo wa IOM amesema kuwa mapigano ya kutumia silaha katika kipindi cha miezi tisa iliyopita yamewaondoa zaidi ya watu milioni sita, na kuongeza kuwa watu milioni tatu ambao tayari wameyakimbia makazi yao nchini Sudan.  

Idadi hiyo mpya inasisitiza umuhimu wa kuimarisha harakati za kimataifa za usaidizi wa kibinadamu katika kile ambacho sasa kinaonekana kuwa ni janga kubwa zaidi la watu kuhama makazi yao duniani. 

Watu waliohamishwa kutoka Sudan wakisaidia na malaka nchini Chad na shirika la IOM. (Maktaba)
IOM
Watu waliohamishwa kutoka Sudan wakisaidia na malaka nchini Chad na shirika la IOM. (Maktaba)

IOM imeendelea kutoa misaada nje na ndani ya Sudan 

Licha ya changamoto zilizoko, Bi. Pope amesema tangu mgogoro huo uanze mwezi Aprili mwaka jana wa 2023, , IOM imekuwa ikisambaza mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka ndani na nje ya nchi ya Sudan, ingawa wafanyakazi wake wengi waliathirika moja kwa moja na wao wenyewe kuyahama makazi yao.  

IOM imejitolea kushughulikia mahitaji haya ya dharura zaidi na inapanua mwitikio wake kwa ombi lake jipya la usaidizi kwa Sudan la dola za milioni 168.  

Mzozo nchini Sudan uliendelea kuwa na madhara makubwa kwa watu wa kawaida. Miundombinu muhimu, ikijumuisha vituo vya huduma vya afya, shule, barabara, na huduma kama vile vyanzo vya umeme na maji, pamoja na mali za mawasiliano ya simu, imeharibiwa.

Bi. Pope amehitimisha kwamba “uharibifu huu umepunguza sana upatikanaji wa huduma muhimu na za kuokoa maisha. Milipuko ya magonjwa, njaa, na utapiamlo ni tishio la kila mara. Zaidi ya hayo, machafuko yameongeza hatari ya unyanyasaji wa kijinsia na kuwaweka wanawake na wasichana katika hatari kubwa.”

Hivi sasa, IOM imefikia karibu watu milioni 1.2 nchini Sudan na nchi jirani kwa msaada wa kuokoa maisha, inayohudumia zaidi ya watu 650,000 nchini Sudan pekee.  

Msaada huo unajumuisha huduma muhimu za ulinzi na afya, makazi ya dharura na vitu vya msaada, msaada wa fedha taslimu, utoaji wa maji safi na vifaa vya usafi, na usafiri muhimu endelevu.  

Halikdhlika iwezesha takribani watu 150,000 kufikia maeneo salama katika nchi jirani ambapo wanaweza kupata huduma za kibinadamu katika hali salama na yenye heshima.