Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na AU walaani ukiukwaji wa mkataba Sudan Kusini

Wakimbizi wa ndani wajengewa makazi ya muda baada ya kutawanywa na machafuko nchini Sudan Kusini. Picha: UNHCR

UN na AU walaani ukiukwaji wa mkataba Sudan Kusini

Muungano wa Afrika AU na Umoja wa Mataifa kwa pamoja wamelaani vikali ukiukwaji wa mkataba uliotiwa saini Disemba 21 mwaka 2017 kwa ajili ya usitishaji uhasama, ulizni wa raia na upatikanaji wa fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu Sudan Kusini.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo , mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika Moussa Faki Mahamat, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, wametoa wito kwa wapiganaji wa pande zote nchini humo kusitisha mara moja mashambulizi, kujizuia kuendesha operesheni Zaidi za kijeshina kuzingatia majukumu yao chini ya mkataba huo wa Disemba 21.

Pia viongozi hao wamehimiza pande zote katika mzozo kutimiza wajibu wao wa kwanza ambao ni ulinzi kwa raia , kuheshimu misingi ya haki za binadamu na sheria za kibinadamu na pia kuhakikisha kwamba fursa ya ufikishaji wa misaada ya kibinadamu inapatikana bila vikwazo vyovyote.

Viongozi hao wamesisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa na jumuiya za kikanda watahakikisha pande kinzani Sudan Kusini zinatekeleza wajibu na majukumu yao na kuhimiza kwamba suluhu pekee ya mzozo nchini humo ni ya kisiasa na pande zote zitawajibu wa kufanikisha hilo.