Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa nchi zinazoendelea kujipanga jinsi ya kujitegemea kiuchumi: Susan Auma

Susan Auma Mang’eni katibu mkuu idara ya ukuzaji wa biashara ndogondogo iliyo ndani ya wizara mpya ya ushirika na ukuzaji wa biashara ndogondogo au ujasiriamali  akihojiwa na Flora Nducha wa Idha ya Kiswahili ya UM jijini New York.
UN News/Anold Kayanda
Susan Auma Mang’eni katibu mkuu idara ya ukuzaji wa biashara ndogondogo iliyo ndani ya wizara mpya ya ushirika na ukuzaji wa biashara ndogondogo au ujasiriamali akihojiwa na Flora Nducha wa Idha ya Kiswahili ya UM jijini New York.

Ni wakati wa nchi zinazoendelea kujipanga jinsi ya kujitegemea kiuchumi: Susan Auma

Ukuaji wa Kiuchumi

Changamoto mbalimbali zinazoendelea duniani ikiwemo athari zilizoletwa na janga la COVID-19 katika mnyororo mzima wa usambazaji wa bidhaa duniani, katika ukuaji wa uchumi, vita inayoendelea nchini Ukraine na majanga ya asili kama ukame vimechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma jitihada za ufadhili wa maendeleo duniani kote na nchi nyingi hasa zinazoendelea zimejikuta katika wakati mgumu.

Ili kuondokana na changamoto kama hizo Susan Auma Mang’eni katibu mkuu wa idara ya ukuzaji wa biashara ndogondogo iliyo ndani ya wizara mpya ya ushirika na ukuzaji wa biashara ndogondogo au ujasiriamali nchini Kenya katika sehemu ya pili ya mahojiano yake na Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili yaliyofanyika wakati wa kongamano la Umoja wa Mataifa la ufadhili kwa ajili ya maendeleo mjini New York Marekani, anasema umewadia wakati kwa nchi zinazoendelea kujipanga upya na kuwa na suluhu mbadala, 

“Kwamba sisi kama nchi zinazoendelea ni lazima tuoene jinsi gani tunaweza kujitegemea na kwanza kuona jinsi tunavyopanga uchumi. Tumekuwa tukipanga uchumi kwa njia ambayo wale ambao wako juu ndio tunaowatilia maanani ambao ni wachache sana ukilinganisha na idadi ya watu wote, lakini wale ambao wako chini kabisa mashinani tumewaacha kando hawajajumuishwa kikamilifu katika uchumi wetu na maendeleo”.

Akaenda mbali zaidi na kusema “Vikwazo vinavyowafanya wasijumuishwe ni pamoja na “ukosefu wa fecha za kufanya biashara, ukosaji wa miundombinu ya uweza kuwafanya kufikia rasilimali hizo.”

Mikakati inayofanywa na Kenya kuwajumuisha wajasiriamali

Bi. Susan Auma amesema “Mikakati ambayo tunafanya kwanza kabisa ni kuwatambua kwamba wao ni muhimu na uchumi wetu hauwezi kukuwa bila wao. Lakini pia tumetambua kwamba hao wafanyabiashara wadogo wao ndio nguzo ya kunyanyua uchumi wote. Nafasi zote za ajira hasa kupitia sekta ya kilimo zinashikiliwa no na imedhihirika kwamba kukiwa na vizuizi kama ukosefu wa ufadhili wa fedha, ukosefu wa miundombinu, ukosefu wa mafunzo yale kamilifu tunaona kwamba wao hawapati fursa ya kuweza kufikia uwezo wao jinsi inavyotakikana.”

Kwa mantiki hiyo amesema sasa kupitia idara hiyo mpya wanaangalia kikamilifu changamoto au vizuizi hivyo na kuona jinsi ambavyo wanaweza kuboresha mazingira ili kuwafanya waweze kupata fecha za kuweza kuboresha biashara zao, kuwaunganisha na masoko, kuweza kuwapatia mafunzo ili kuwawezesha kufanya biashara bora zaidi na pia kuangalia nini cha kukiimarisha ili kuweka mazingira bora zaidi ya biashara.

Amesema hilo litawezekana kwa “Kuleta wafadhili wote pamoja na kuweza kupanga pamoja sababu changamoto ambayo imekuwa haizai matunda ni kwamba kila mtu amekuwa kifanya mambo kivyake, wafadhili wamekuwa wakifanya jitihada kivyao, sekta binasi vivyohivyo na pia idara tofautotofauti za serikali zimekuwa zikifanya kivyake. Na tukiendelea kufanya hivyo hatuwezi kuboresha mazingira kikamilifu kuweza kusongesha mbele biashara ndogondogo, ziweze kukua, kupata faida.”

Ameongeza kuwa hilo likibadilika na biashara hizo ziweze kupata faida basi zitaweza kuchangia pakubwa katika kukuza uchumi na kuboresha hali ya maisha hasa nchini Kenya.

Mboga zikiandaliwa wakati wa mafunzo kwa wakulima na wanabiashara huko Taita nchini Kenya
© FAO/Fredrik Lerneryd
Mboga zikiandaliwa wakati wa mafunzo kwa wakulima na wanabiashara huko Taita nchini Kenya

Ni wakati wa kuhoji mwenendo wetu wazaa matunda?

Bi. Susan Auma hata hivyo amesema pamoja na kutegemea ufadhili wa kifedhja hasa kutoka nje sasa ni wakati wa kubadili mwelekeo “ Wakati umefika wa sisi kujiuliza maswali na kuona kwamba huu mwenendo ambao tumekuwa tunaufuata je unazaa matunda ama la?. Kwa hivyo sisi ambao tunatoka katika bara la Afrika na hasa sisi ambao tunatoka Kenya tunasema kwamba changamoto kubwa sana ni jinsi tunavyopanga utekelezaji wa uchumi. Tunapaswa kutambua uwezekano wa kiuchumi katika kila sehemu yetu na jinsi ya kukuza huu uchumi kupitia mbinu zetu za Kiafrika, kupitia utamaduni wetu, jinsi ambavyo tumeweza kuishi na mnyororo wa thamani wa kitamaduni ambao tuko nao.”

Kisha akasema “sasa tuangazie uchumi na si kutokana na ukosefu au changamoto zetu bali na fursa tulizo nazo zilizopo ambazo Mungu ametujalia. Fursa hizo ni pamoja kwa ukweli kwamba watu wetu wanabidii sana, hawataki kupangwa katika njia mpya na linapokuja suala la minyororo ya thamani ya kitamaduni watu wetu wanajua na kutegemea kilimo na sasa kuna teknolojia ya kutumia simu za rununu kama M-pesa, na Kenya imedhihirisha kwamba tukitumia hii teknolojia twaweza kuwafikia watu wengi.”

Soundcloud

Teknolojia ni jawabu mujarabu

Afisa huyo wa serikali ya Kenya amesema na kwa kutambua fursa inayoletwa na teknolojia basi teknolojia hiyo inaweza kutumika kwa mapana zaidi ili kutatua changamoto zilizopo.

“Na sasa tunachojaribu kuona ni jinsi tutakavyowachukua watu wa mashinani na maazimio yao tutalete juu katika uongozi ili tuweze kujikita nayo. Na tukiandaa ufadhili tusake mbinu ambayo inatambua na kujielekeza zaidi katika upande wa fursa.”