Tukidhibiti taka tutanusuru makazi yetu:UN-HABITAT

1 Oktoba 2018

Taka zilizokithiri katika makazi ya binadamu ni lazima zidhibitiwe la sivyo zitaweka hatarini sio tu mazingira bali afya zao. Wito huo umetolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT hii leo katika kuadhimisha siku ya makazi duniani.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “udhibiti wa taka katika manispaa” na hafla ya maadhimisho ya mwaka huu kimataifa yamefanyika kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Nairobi Kenya.

UN-HABITAT inasema taka ni changamoto ya kimataifa inayomuathiri kila mtu, na kiwango cha taka kinachozalishwa na watu binafsi kinaongezeka kila uchao na mara nyingi taka hizo zinagharimu serikali za manispaa kiasi kikubwa cha bajeti zao.

Shirika hilo limeongeza kuwa uzembe wa kukusanya taka hizo na kuzitupa katika majalala yanayohusika kunaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya kwa kuwa na majalala yanasiyodhibitiwa na uchomaji holela wa taka hizo, lakini pia kunachangia uchafuzi wa mazingira, hewa na maji.

Sasa UN-HABITAT inasisitiza kuwa kubadili tabia na kupunguza kiwango cha taka, ikiwemo kuacha kutupa taka hizo hovyo, kuboresha huduma za ukusanyaji taka, kuongeza hukla ya kutumia tena baadhi ya vitu kama mifuko, kuongeza ufadhili, kuwa na mipango maalumu na maeneo ya kutupa taka kunaweza kusaidia kuboresha hali ya sas aya udhibiti wa takataka na kuokoa fedha kwa kuwa na miji yenye busara dhidi ya taka.

 

Siku ya makazi duniani hufanyika kila mwaka Oktoba Mosi na ilitengwa mahsusi na Umoja wa Mataifa ili kutathimini hali ya miji na makazi na haki ya msingi ya kuwa na makazi stahiki kwa wote.

Pia siku hii inakumbusha kwamba kila mtu ana uwezo na wajibu wa aumua mustakabali wa miji na makazi yetu.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter