Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania kuendelea kusongesha ajenda za UN- Balozi Kattanga

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Hussein Kattanga (kulia) akiwasilisha nyaraka za utambulisho kwa Katibu Mkuu wa UN António Guterres jijini New York, Marekani tarehe 17 Aprili 2023.
UN/Eskinder Debebe
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Hussein Kattanga (kulia) akiwasilisha nyaraka za utambulisho kwa Katibu Mkuu wa UN António Guterres jijini New York, Marekani tarehe 17 Aprili 2023.

Tanzania kuendelea kusongesha ajenda za UN- Balozi Kattanga

Masuala ya UM

Mwakilishi Mpya wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Hussein Kattanga amewasilisha nyaraka za utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kushika wadhifa huo tarehe 3 mwezi Januari mwaka huu wa 2023.

Soundcloud

Pamoja na nyaraka hizo alizowasilisha kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Balozi Kattanga amewasilisha pia salamu kutoka kwa Rais Samia huku Katibu Mkuu akisema Tanzania ni nchi ambayo iko moyoni mwake.

Idhaa ya Kiswahili Umoja wa Mataifa ilitumia fursa hiyo kuzungumza na Balozi Kattanga ili kufahamu ujumbe aliowasilisha kwa Katibu Mkuu Guterres kutoka kwa Rais Samia.

Tweet URL

Balozi Kattanga: Ujumbe ambao Rais amenipatia ni kwamba Tanzania bado ni mwanachama mwenye nguvu kwenye kushiriki masuala yote ya kulinda amani, maendeleo na haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo ujumbe rasmi ni kwamba Tanzania ni mshiriki na nafasi yake ni maalum kwenye masuala hayo.

Tanzania tumejiunga na Umoja wa Mataifa mwaka 1961 baada ya uhuru. Umuhimu wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya amani na usalama, maendeleo ya binadamu na masuala ya haki za binadamu, nadhani kila mmoja, kila mtanzania anatambua. Dunia kadri ilivyokuwa inaenda ilikuwa inabadilika na kuwa kijiji. Kwa hiyo umuhimu wa kuwa na amani na utulivu kwa maendeleo ya binadamu ilikuwa ni muhimu zaidi hasa kwenye majukwaa ya Umoja wa Mataifa.

Idhaa ya UN: Na Je Umoja wa Mataifa umekuwa na mchango gani kwa Tanzania?

Balozi Kattanga:Mchango uko wazi na bayana kwa sababu ukiangalia Umoja wa Mataifa unavyofanya kazi zake kwa mfano kupitia taasisi zinazofanya kazi kwenye nchi zetu. Mfano nchini Tanzania ukizungumzia masuala ya watoto, unazugumzia UNICEF, ukizungumzia maendeleo ni UNDP, ukizungumzia afya kuna WHO. Kwa hiyo Umoja wa Mataifa uko ndani ya mioyo na mifumo ya maisha ya watanzania.

 Idhaa ya UN: Vipi hali ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu au SDGs yanayofikia ukomo mwaka 2030?

Balozi Kattanga: Malengo haya ya maendeleo endelevu, SDGs yameingizwa katika mipango ya maendeleo ya Tanzania. Mfano Dira ya Taifa ambayo imefanyiwa mapitio hivi karibuni,Mipango ya Muda wa Kati ya miaka mitano, lakini pia mipango ya kisekta. Hivyo unaona ni vipi tumetumbukiza masuala hayo ya kimataifa kwenye mifumo yetu ya kitaifa. Ukiangalia utendaji na matarajio ni kwamba mpaka sasa tumefikia asilimia 51 ya malengo, ambacho ni kiwango cha juu sana kati ya nchi zinatekeleza SDGs.

Balozi Hussein Kattanga, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye UN akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya UN jijini New York, Marekani.
UN News
Balozi Hussein Kattanga, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye UN akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya UN jijini New York, Marekani.

Idhaa ya UN: Na nini mchango wa Tanzania kwenye operesheni za ulinzi wa amani za  Umoja wa Mataifa?

Balozi Kattanga: Mchango wa Tanzania ni mkubwa na ukiangalia iko katika nchi 10 bora za uchangiaji kwenye ulinzi wa amani. Tuko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lebanon. Nadhani mnaona mchango wetu kwenye zile nchi 10 bora zinazoshiriki kwenye ulinzi wa amani.

Idhaa ya UN: Na upi mpango wa kusongesha lugha ya Kiswahili ambayo ni ya kimataifa hivi sasa ili iwe moja lugha rasmi za Umoja wa Mataifa?

Balozi Kattanga: Rais Samia Suluhu Hassan na marais waliomtangulia wamekuwa ni vinara wa jambo hili. Kwetu sisi watanzania hii si lugha tu ya kuzungumza, bali pia ni lugha ya kujenga udugu, maelewano  mshikamano na amani. Kwetu sisi ni lugha ya amani. Kwetu sisi ujumbe tunataka ufikie watu wengi ni kwamba tulianza Tanzania kwenye ngazi ya nchi, kila mtanzania azungumze kiswahili. Kisha tukaenda kwa jirani nchi zinazotuzunguka, kiswahili kinazungumza. Baada ya hapo tumeingia kwenye Jumuiya kama ya Afrika Mashariki, EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC na tayari kimefika Muungano wa Afrika, AU. Sasa jukwaa lililobakia ni Umoja wa Mataifa. Tumeenda taratibu lakini kimkakati na tutafika na wakati wa kipindi ninahudumu hapa, hiyo itakuwa ni ajenda muhimu.