Baraza la Usalama lalaani mauaji ya walinda amani huko DRC
Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali mauaji ya walinda amani wa Tanzania huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Japan ambayo ndiyo Rais wa Baraza la Usalama la Umoja kwa mwezi huu wa Disemba imesoma taarifa ya wajumbe wa baraza hilo ikielezea masikitiko yao kufuatia vifo hivyo vya walinda amani 15 kutoka Tanzania huku wengine wapatao 53 wakijeruhiwa.
Katika taarifa hiyo Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Japan kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Yasuhisa Kawamura amesema wajumbe wamelaani vikali mashambulio hayo na uchochezi dhidi ya walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO kunakofanywa na watu waliojihami.
Wametoa wito kwa serikali ya DRC kuhakikisha watekelezaji wanachukuliwa hatua na kusisitiza matakwa yao kuona vikundi vyote vilivyojihami vinasitisha aina zote za ghasia.
Ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa walinda amani ambao wanaweka rehani maisha yao kila siku ili kulinda amani duniani.
Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza kuunga mkono kazi za Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko DRC katika kutekeleza majukumu ya MONUSCO nchini humo.