Wakati umefika Kiswahili kiwe lugha rasmi ya UN - Tanzania

21 Oktoba 2019

Vikao vya kamati ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa vikiendelekea kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani, Tanzania imerejelea wito wake wa kutaka lugha ya Kiswahili iwe miongoni mwa lugha rasmi za chombo hicho chenye jumla ya wanachama 193.

Akihutubia kikao hicho leo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Modest Mero amesema wito huo wa taifa hilo la Afrika Mashariki unazingatia ukweli ya kwamba Kiswahili hivi sasa ni lugha ya kiafrika inayozungumzwa na takribani watu milioni 500 kote duniani.

“Na kama hiyo haitoshi tayari lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi kwenye Muungano wa Afrika, AU, Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Bunge la Afrika na hivi karibuni ilitangazwa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC. Kiswahili pia hutumika kwenye matangazo ya vyombo vikubwa vya habari vya Televisheni na Redio barani Afrika, Ulaya, Urusi, Amerika, Asia na Mashariki ya Mbali,” amesema Balozi Mero wakati akihutubia wajumbe wa kamati hiyo ya 4 ambayo ilikuwa na mjadala kuhusu hoja ya masuala ya habari.

UNICS ziimarishwe

Balozi Mero alitumia hotuba hiyo pia kuzungumzia uhusiano baina ya vituo vya habari vya Umoja wa Mataifa, UNICS na serikali na taasisi nyinginezo akisema kuwa, “ijapokuwa vituo hivyo vimeanzisha uhusiano mzuri na ubia na taasisi za serikali na vyombo vya habari vya umma, bado havina shughuli za kutosha kueleka mashinani ili viweze kuhabarisha kwa kina wananchi kuhusu shughuli za Umoja wa Mataifa.”

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa akasema, “ni kwa mantiki hiyo kuna umuhimu wa Idara ya Mawasiliano kwa Umma, DGC iandae mfumo bora wa kuwezesha upashaji wa taarifa kwa umma na ushirikishi wa umma.”

Pamoja na kuwepo kwa muundo thabiti, Balozi Mero ametaka vituo  hivyo ikiwemo kile kilichopo Tanzania kipatiwa rasilimali za kutosha ili viweze kutekeleza majukumu yake ambayo vituo hivyo hupatiwa na Kamati hiyo ya 4 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Balozi Modest Mero, mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili.
UN News Kiswahili/ Patrick Newman
Balozi Modest Mero, mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili.

YPP ijumuishe nchi zizungumzazo Kiswahili

Akizungumzia mitihani ya kila mwaka ya mpango wa kuajiri vijana wabobezi kwenye Umoja wa Mataifa, YPP, Balozi Mero amesema, “kuna umuhimu wa kuweka kwenye orodha ya nchi shiriki, mataifa yanayozungumza lugha ya Kiswahili ili kujenga uwezo wa kitengo cha habari za Kiswahili ndani ya Umoja wa Mataifa. Hii itawezesha kitengo hicho kufanya kazi yake kwa ufanisi kwa ajili ya wazungumzaji wa Kiswahili kupitia Televisheni, Redio na mitandao ya kijamii.”

Nafasi ya Radio na Televisheni bado ni muhimu

Katika hotuba  yake, Balozi Mero amesisitiza kuwa pamoja na kuwepo kwa teknolojia za kisasa za upashaji habari, “Tanzania inaungana mkono na wanachama wengine juu ya umuhimu wa teknolojia za kisasa zilizopo katika mawasiliano duniani ambako matumizi ya njia za zamani kama matangazo ya redio na televisheni yanasalia kuwa mbinu inayotumika zaidi kwa vizazi vingi duniani.”

Hata hivyo amesema kuna umuhimu wa mataifa yote kuweka kanuni za udhibiti hususan matumizi holela ya taarifa za umma na upashaji habari usio sahihi, ambavyo amesema vinaweza kuwa na madhara makubwa kwa jamii.

Ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na nchi wanachama zizingatie maazimio na maamuzi yaliyopitishwa na kuweka maadili ambayo yanaweza kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya  juu vya usahihi, maadili na uwajibikaji ili kuepusha matumizi holela ya taarifa na njia za mawasiliano kinyume na sheria ya kimataifa.

Kamati ya 4 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inahusika na masuala kadhaa ikiwemo habari, hoja ya Palestina na kutokomeza ukoloni.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter