Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yafunga kambi ya Kamango huko Beni, DRC

Ingawa kambi ya kijeshi ya MONUSCO huko Kamango imefungwa, MONUSCO bado iko katika eneo hilo na inaendelea kufanya kazi kupitia mawasiliano na ulinzi wa zana za raia ambazo imeweka.
MONUSCO / Ado Abdou et Papy Martial Mukeba
Ingawa kambi ya kijeshi ya MONUSCO huko Kamango imefungwa, MONUSCO bado iko katika eneo hilo na inaendelea kufanya kazi kupitia mawasiliano na ulinzi wa zana za raia ambazo imeweka.

MONUSCO yafunga kambi ya Kamango huko Beni, DRC

Amani na Usalama

Kambi ya Kamango iliyokuwa inamilikiwa na kikosi cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO imefungwa baada ya kukamilisha jukumu lake.

Kambi hiyo iliyoko kilometa 80 kaskazini-magharibi mwa mji wa Beni jimbo la Kivu Kaskazini ilianzishwa miaka 10 iliyopita kukabili vitisho kutoka waasi wa ADF na imefungwa rasmi tarehe 6 mwezi huu. 

Kwa mujibu wa chapisho la MONUSCO, kambi hiyo sasa imekabidhiwa kwa mamlaka za eneo hilo ambapo Chifu wa Kata ya WAtalinga ilimo kambi hiyo ameshukuru kwa kazi nzuri iliyofanywa na MONUSCO ya kurejesha usalama kwa raia. 

Ijapokuwa kituo hicho kimefungw,a MONUSCO itaendelea kusalia kwenye eneo hilo kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano na usalama kwa raia. 

MONUSCO inasema vifaa na miundombinu iliyokuwemo itatumiwa na mamlaka za eneo hilo na kufungwa kwa kambi hiyo kunakwenda sambamba na mpango wa mpito wa kuanza kukabidhi majukumu ya usalama kwa serikali ili hatimaye ujumbe huo uondoke DRC. 

Chifu wa Watalinga, Mwami Saambili Bamukoka akizungumzia hatua ya kufungwa kwa kituo hicho amesema “kwa kiasi kikubwa MONUSCO imesaidia kuimarisha usalama eneo hili. Tunashukuru kwa kazi ya vikosi mbali mbali vilivyoshirikiana nasi hapa. Tunaweza kusema sasa hali ya usalama ni nzuri.” 

Ameongeza kuwa wao ni sehemu ya mji wa Beni na ingawa kwingineko wanakumbwa na changamoto za usalama, wao enoe lao ni tulivu. 

Kwa upande wale Odette Zawadi ambaye ni Rais wa shirika la kiraia la kuchochea maendeleo Watalinga amesema mchango wa MONUSCO kwenye usalama wa eneo lao ni dhahiri kwa kuwa hivi sasa raia wanaweza kuendesha shughuli zao bila hofu, wanawake wanaweza kwenda shambani bila kushambuliwa. 

Amesema “ninavyozungumza, hapa kuna amani, wananchi wanaenda mashambani, kila mtu anafanya shughuli zake kwa uhuru. Hii ni kumbukumbu nzuri sana ya uwepo wa MONUSCO hapa, kwa sababu sasa tunajua bila amani hakuna kinachoweza kufanyika.”