Walinda amani wanawake kutoka Tanzania waleta nuru kwa wanawake DRC

4 Machi 2019

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO wamezungumzia jinsi ambavyo mafunzo ya ujasiriamali wanayowapatia wanawake nchini humo yamebadili maisha yao.

Miongoni mwa walinda amani hao ni Kapteni Mercy Kayonde aliyepo eneo la Mavivi, huko Beni jimbo la Kivu Kaskazini ambaye katika mahojiano kwa njia ya simu na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amefafanua kwa kina kile wanachofanya akisema, “tumeanzisha vikundi tofauti tofauti kwa ajili ya kuwasaidia kama kujifunza jinsi ya kupanda bustani ndogo ndogo ambazo zitawasaidia kujikimu kwenye maisha yao ya kawaida. Vile vile tumewafundisha ujasiriamali kama ushonaji wa nguo. Vitu vyote  hivyo tumewafundishi ili angalau waweze kujisaidia badala ya kukaa bila kufanya chochote.”

Alipoulizwa baada ya mafunzo, wanawake hao wanapata wapi mtaji, Kapteni Kayonde amesema kwamba, “kama suala la bustani hizo ndogo ndogo tunawafundisha jinsi ya kuandaa shamba na mbegu tunawapatia kabisa. Tunawafundisha jinsi ya kuandaa shamba, upandaji wa mbegu na tunawafuatilia kila siku kujua bustani zao zinaendeleaje. Suala la kushona nguo, sisi wanajeshi mafundi cherehani tunao kwa hiyo wanakuja wanajifunza na tumejitahidi tumewapatia cherehani hizo ili wakaanze kazi rasmi ya kujipatia kipato.

Kwa mujibu wa Kapteni Kayonde, kilimo cha mboga mboga kimesaidia kwa kuwa mboga hizo zinalika Beni na pia wanauza na kupata kipato.

Halikadhalika amesema miradi ambayo wameianzisha imesaidia wanawake hao kutokwenda mbali kwa ajili ya kilimo na kwamba hata mwenye eneo dogo wamewafundisha wapande mbogamboga kwenye mifuko ya nailoni, wanapanda mbegu na kumwagilia hadi wanavuna na kwa kufanya hivyo wanakuwa mbali na vikundi vya maadui.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter