Kinachotokea Beni kinatuchukiza- Zerrougui

26 Novemba 2019

Umoja wa Mataifa umesema mashambulizi dhidi ya ofisi za makao yake makuu huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ni jambo linalochukiza wakati ambapo umoja huo unakabiliwa na maandamano ya watu waliokata tamaa baada ya kushambuliwa na vikundi vilivyojihami.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC Leila Zerrougui amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka DRC.

Kauli yake inafuatia kushambuliwa kwa ofisi za makao makuu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO zilizoko mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini jumatatu ya tarehe 25 mwezi huu wa Novemba.

Katika tukio hilo watu wenye hasira walitia moto ofisi za Umoja wa Mataifa na ukumbi wa mikutano wa mji wa Beni wakidai kuwa jeshi la serikali na walinda amani wameshindwa kuzuia shambulio la mwishoni mwa juma ambalo kwa mujibu wa vyombo vya habari lilifanywa na kikundi cha waasi cha Allied Democratic Forces, au ADF.

Akifafanua Bi. Zerrougui amesema, “eneo hili ndilo limeathiriwa kwa Ebola n ani eneo ambalo kwa miaka 20 sasa limekuwa na shida kubwa ambazo raia ndio wamegharimika zaidi.”

Amesema “Beni ni eneo la msitu na si rahisi kufikika na raia wametapakaa katika maeneo mengi, vijiji na si rahisi kila mtu kupatiwa ulinzi.”

Bi. Zerrougui ambaye pia ndiye mkuu wa MONUSCO amesema kuwa, “Unapokuwa na jukumu na kisha unakuwa na jukumu la kukabili mashambulizi, watu wanatarajia wewe umsambaratishe adui. Lakini si rahisi kumsambaratisha adui. Hii ni kwa sababu unakabiliana na kikundi cha kigaidi kinachotumia mbinu za kigaidi, kushambulia raia usiku wa manane.”

Kutokana na kushamiri kwa maandamano, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kwenye ujumbe huo wamehamishiwa maeneo mengine salama.

Beni ni kituo muhimu cha Umoja wa Mataifa na serikali ya DRC katika harakati zao za kukabili mlipuko wa ebola uliodumu kwa zaidi yam waka mmoja sasa na ambao tangu Agosti mwaka jana wa 2018 umesababisha vifo vya watu takribani 3,000.

Takribani walinda amani 16,000 wanahudumu MONUSCO ambapo huko Beni kuna walinda amani 557 kutoka Malawi, na kikosi cha polisi kutoka India chenye maafisa 150 ilihali walinda amani 150 kutoka Tanzania wamepiga kambi karibu na uwanja wa ndege wa Beni.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter