Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunatarajia kufanya kazi na Equatorial Guinea na Tanzania katika majaribio ya chanjo dhidi ya Marburg- WHO

Wataalamu wa maabara wakifanya utafiti kwenye Maabara ya Utafiti ya Baney huko Malabo nchini Equatorial Guinea (Maktaba)
WHO
Wataalamu wa maabara wakifanya utafiti kwenye Maabara ya Utafiti ya Baney huko Malabo nchini Equatorial Guinea (Maktaba)

Tunatarajia kufanya kazi na Equatorial Guinea na Tanzania katika majaribio ya chanjo dhidi ya Marburg- WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limesema kamati yake kuhusu chanjo imeshapitia ushahidi wa matumizi ya chanjo aina 4 dhidi ya ugonjwa wa Marburg na kwamba maandalizi ya majaribio yamekamilika.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo hii leo huko Geneva, Uswisi akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano unaofanyika kila jumatano kutoa muhtasari na mwelekeo wa masuala ya afya duniani.

Itifaki za majaribio zimekamilika

Amesema itifaki za majaribio zimekamilika na wadau wa WHO wako tayari kusaidia majaribio ya chanjo hizo dhidi ya ugonjwa huo ambao hivi karibuni umeripotiwa Equatorial Guinea na Tanzania.

“Tunategemea kushirikiana na serikali hizi mbili ili kuanza majaribio na kusaidia kuzuia maambukizi zaidi na vifo, halikadhalika kuzuia milipuko zaidi katika siku za usoni,” amesema Dkt. Tedros.

Equatorial Guinea kuna taarifa za wagonjwa wengine

Amesema  huko Equatorial Guinea WHO na wadau wake wanasaidia Wizara ya Afya kukabili mlipuko wa Marburg hasa katika kusaidia kubaini wagonjwa, kutoa tiba na kushirikisha jamii.

Tanzania imethibitisha mlipuko wa kwanza kabisa nchini humo wa ugonjwa wa virusi vya Marburg
© WHO/Benjamin Sensasi
Tanzania imethibitisha mlipuko wa kwanza kabisa nchini humo wa ugonjwa wa virusi vya Marburg

“Tumesaidia pia kuanzisha vituo vya matibabu kwenye maeneo yaliyoathirika. Idadi ya wagonjwa inasalia ile ile 9 ambapo kati yao 7 wamefariki dunia katika majimbo  matatu,” amesema Dkt. Tedros akieleza kuwa hata hivyo majimbo hayo yanatenganishwa na umbali wa kilometa 150 jambo linalodokeza kuwa ugonjwa umesambaa eneo kubwa.

WHO ina taarifa ya kuweko kwa wagonjwa wengine hivyo imeomba serikali ya Equatorial Guinea kuwasilisha rasmi WHO taarifa hizo.

Tanzania idadi ya wagonjwa haijabadilika

Kwa upande wa Tanzania nako asema idadi ya wagonjwa waliothibishwa ni wale wale 8 na waliokufa ni 5 na waliosalia watatu wanapatiwa matibabu katika kituo cha afyana kwamba hadi sasa wagonjwa hao wote wako katika mkoa mmoja wa Kagera, kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Tayari WHO na wadau kama vile UNICEF, kituo cha udhibiti magonjwa cha Marekani CDC na madaktari bila mipaka, MSF wanasaidia serikali kuziba pengo la hatua za kukabili mlipuko huo.

Dkt. Tedros amekumbusha kuwa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg ni kumbusho lingine ya kwamab “tunaweza kulinda afya ya binadamu iwapo tutalinda pia afya ya wanyama na sayari yetu ambayo inaendeleza uhai wote. Tunaita hii mfumo wa Afya Moja.”