Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna tena ugonjwa wa Marburg nchini Equatorial Guinea: WHO

WHO yatangaza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg umetokomezwa huko Equatorial Guinea.
© WHO
WHO yatangaza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg umetokomezwa huko Equatorial Guinea.

Hakuna tena ugonjwa wa Marburg nchini Equatorial Guinea: WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO kanda ya Afrika limetangaza rasmi kumalizika kwa ugonjwa wa Marburg nchini Equatorial Guinea baada ya kutogundulika uwepo wa mgonjwa yeyote kwa muda wa siku 42 tangu mgonjwa wa mwisho kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Taarifa ya pamoja kutoka mjini Brazzaville nchini Kongo na Malabo Equatorial Guinea imesema tangu kutangazwa kulipuka kwa ugonjwa huo Februari 13, 2023 jumla ya watu 17 walithibitishwa na maabara kuugua, vifo 12 vilirekodiwa na wagonjwa wanne walipona virusi hivyo na wameandikishwa katika mpango wa manusura ili kupokea usaidizi wa kisaikolojia na mwingine wowote baada ya kupona.

Mkurugenzi wa WHO Afrika Dk Matshidiso Moeti amepongeza timu za wataalamu wa Afrika “ Wakati magonjwa ya mlipuko yanaendelea kuwa tishio kubwa la kiafya barani Afrika, tunaweza kuunga mkono utaalamu unaokua wa kanda katika kukabiliana na dharura ya kiafya, kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kulinda afya na kuepusha kupoteza maisha.”

WHO ilivyoshirikiana na nchi kumaliza mlipuko huo

Ili kuunga mkono na kuisaidia Equatorial Guinea kupambana na mlipuko huo, WHO ilituma wataalamu wa magonjwa ya mlipuko, usimamizi wa kliniki, shughuli za afya, vifaa, mawasiliano ya hatari na kuzuia na kudhibiti maambukizi.

WHO ilifanya kazi na mamlaka ya afya ya nchi hiyo kuanzisha kituo cha matibabu, kutoa vifaa vya matibabu ikiwa ni pamoja na dawa za kuzuia virusi na wahudumu wa afya waliofunzwa katika nyanja muhimu za kudhibiti milipuko.

WHO imepongeza wafanyakazi wa afya wa nchi hiyo kwa juhudi za kumaliza ugonjwa huo mbaya uliopo katika familia/ kundi moja na magonjwa ya mlipuko kama virusi vya Ebola.

“Kazi ngumu ya wafanyakazi wa afya wa Equatorial Guinea na usaidizi wa mashirika washirika imekuwa muhimu katika kumaliza mlipuko huu. WHO inaendelea kufanya kazi na nchi kuboresha hatua za kugundua na kukabiliana na magonjwa ya milipuko,” ameongeza Dk Moeti.

WHO pia iliunga mkono juhudi za mamlaka katika nchi jirani za Cameroon na Gabon kuongeza utayari na kukabiliana na mlipuko.

WHO itaendelea kushirikiana na Equatorial Guinea

Ingawa mlipuko huo umeisha, WHO inaendelea kufanya kazi na Equatorial Guinea kuimarisha hatua za kujilinda kama vile ufuatiliaji na upimaji ili kuwezesha hatua za haraka iwapo virusi hivyo vitatokea.

Pia wanaendelea na utoaji wa mafunzo kuhusu mlipuko huo leongo ni kusaidia kuimarisha uwezo wa kujitayarisha.

Virusi vya Marburg huingia kwa binadamu kutoka kwenye matunda yaliyoliwa na popo na huenea kati ya wanadamu kwa kugusana moja kwa moja na maji ya mwili ya watu walioambukizwa, uso kwa uso au kushika eneo aliloshika mtu mwenye virusi.

Barani Afrika, mlipuko wa kwanza wa Marburg ulirekodiwa nchini Afrika Kusini mwaka wa 1975, ukifuatiwa na wengine wawili nchini Kenya katika miaka ya 1980. Tangu wakati huo milipuko imeripotiwa nchini Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ghana, Guinea na Uganda, na hivi karibuni Equatorial Guinea na Tanzania.