Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yachunguza ugonjwa wa virusi vya Marburg Guinea

Nchini Guinea sasa kumeripotiwa homa ya virusi vya Marburg (maktaba)
WHO/Junior D. Kannah
Nchini Guinea sasa kumeripotiwa homa ya virusi vya Marburg (maktaba)

WHO yachunguza ugonjwa wa virusi vya Marburg Guinea

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya wanashirikiana na serikali ya Guinea kuchunguza ugonjwa mpya unaosababishwa na virusi vya Marburg ambao kwa mara ya kwanza umegundulika huko Afrika magharibi. 

Katika mkutano wake na vyombo vya habari mjini Geneva, Uswisi hii leo Mkurugenzi Mkuu wa WHO DKT. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema “ijumaa iliyopita ya tarehe 6 mwezi huu wa Agosti Waziri wa Afya wa Guinea aliitarifu rasmi WHO kuhusu kuwepo kwa mgojwa aliyegundulika kuwa na virusi vya Marburg kusini magharibi mwa nchi hiyo ambaye alifariki dunia siku 8 baada ya kubainika kuwa na dalili za ugonjwa huo.”

Marburg ni aina tofauti ya virusi ikilinganishwa na virusi vya Corona au COVID-19 lakini kuna ufanano kwenye namna vinavyoshughulikiwa, wagonjwa wanavyotengwa, uchunguzi wa watu wote mgonjwa aliokutana nao unafanyika na wanawekwa karantini, pamoja na kuishirikisha jamii katika kukabiliana nao.
 
Jumla ya watu 150 wametambuliwa kuwa walikutana na mgonjwa aliyefariki dunia na wanafuatiliwa, idadi hiyo ni pamoja na wanafamilia watatu wa marehemu na mhudumu wa afya ambaowote wameainishwa kuwa wapo hatarini zaidi kwa kuwa walikuwa karibu na mgonjwa wa Marburg.
 
Mpaka sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa ya ugonjwa wa Marburg, japo kuna chanjo mbalimbali ambazo zinaendelea kutengenezwa na WHO kwa kushirikiana na wadau wengine wanaangalia fursa ya kuweza kuzipata iwapo kutakuwa na mlipuko wa ugonjwa huo.