Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yathibitisha mlipuko wa kwanza nchini humo wa homa ya Marburg

Tanzania imethibitisha mlipuko wa kwanza kabisa nchini humo wa ugonjwa wa virusi vya Marburg
© WHO/Benjamin Sensasi
Tanzania imethibitisha mlipuko wa kwanza kabisa nchini humo wa ugonjwa wa virusi vya Marburg

Tanzania yathibitisha mlipuko wa kwanza nchini humo wa homa ya Marburg

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO limesema linasaidia harakati za Tanzania za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa homa ya Marburg ulioripotiwa kaskazini magharibi mwa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Taarifa iliyotolewa na WHO huko Brazaville, Jamhuri ya Congo na Dar es salaam nchini Tanzania inasema serikali ilithibitisha kuweko kwa mlipuko huo ambao ni mara kwanza kukumba nchi hiyo na tayari kuna vifo vitano kati ya watu 8 walioambukizwa ugonjwa huo.

“Maabara ya kitaifa ya afya ya umma ilichunguza sampuli ili kubaini sababu ya ugonjwa baada ya watu wanane kupata dalili kama vile homa, kutapika, kutokwa damu na figo zao kushindwa kufanya kazi,” imesema taarifa hiyo.

Miongoni mwa waliokufa ni mhudumu wa afya huku waliosalia watatu wanapatiwa matibabu.

Jumla ya watu 161 waliobainika kuwa waambata wa waliokufa na wanaopatiwa matibabu tayari wametambuliwa na wanafuatiliwa kwa karibu.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema juhudi za mamlaka za afya nchini Tanzania za kubaini sababu za ugonjwa hu ni kiashiria dhahiri cha azma ya taifa hilo kuchukua hatua dhidi ya mlipuko huo.

Tumepeleka wataalamu Kagera

“Tunashirikiana na serikali kuongeza mikakati ya udhibiti na kukomesha kusambaa kwa virusi hivyo vya Marburg na hatimaye kumaliza mlipuko huo haraka iwezekanavyo,” amesema Dkt. Moeti.

Mathalani WHO inasaidia Wizara ya Afya ya Tanzania kupeleka mkoani Kagera timu ya dharura ya wahudumu wa afya ili kufanya uchunguzi zaidi wa kitabibu.

Timu hiyo itajikita kwenye kusaka wagonjwa katika jamii halikadhalika vituo vya afya ili kuona kama kuna waambata zaidi na kuwapatia huduma inayostahili.

Ingawa Tanzania haijawahi kuwa na mgonjwa wa Marburg, tayari imekuwa na uzoefu wa hatua dhidi ya coronavirus">COVID-19, kipindupindu, denge katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Tathmini ya kimkakati iliyoendeshwa na WHO mwezi Septemba mwaka 2022 ilionesha kuwa taifa hilo liko kwenye hatari kubwa ya kupata mlipuko wa magonjwa ya maambukizi.

Marburg ni nini na je kuna tiba?

Ugonjwa wa virusi vya Marburg unaaambukiza kwa kiwango kikubwa na husababisha  homa, kutokwa na damu na kiwango cha vifo ni takribani asilimia 88.

Mgonjwa anapata dalili za homa kali ghafla, kichwa kuuma sana na kujisikia mchovu.

Virusi vya Marburg huambukizwa kwa binadamu kutoka kwa popo na maambukizi ya binadamu kwa binadamu ni kupitia kugusa majimaji ya mgonjwa yaliyoko mwilini au kwenye sakafu, kuta na kwingineko.

Hadi sasa hakuna chanjo au tiba zilizothibitishwa dhidi ya virusi hivyo. Hata hivyo huduma ya usaidizi kama vile maji ya kuongeza nguvu mwilini na tiba kwa dalili mahsusi vinaweza kuongeza uwezo wa mgonjwa kupona.