Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaitisha mkutano wa dharura baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Marburg nchini Equatorial Guinea

Nchini Guinea sasa kumeripotiwa homa ya virusi vya Marburg (maktaba)
WHO/Junior D. Kannah
Nchini Guinea sasa kumeripotiwa homa ya virusi vya Marburg (maktaba)

WHO yaitisha mkutano wa dharura baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Marburg nchini Equatorial Guinea

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO hii leo limeitisha mkutano wa dharura wa muungano wa chanjo ya virusi vya Marburg ili kujadili mlipuko mpya wa ugonjwa huo nchini Equatorial Guinea.

Hapo jana Equatorial Guinea ilithibitisha mlipuko wa kwanza wa ugonjwa huo baada ya kuendesha upimaji wa awali kufuatia vifo vya takriban watu tisa katika mkoa wa Kie Ntem ulioko Magharibi mwa nchi hiyo na kubaini kuwepo kwa homa hiyo ya virusi vya haemorrhagic.

Muungano huo wa chanjo ya virusi vya Marburg au MACVAC unajumuisha viongozi kwenye sekta ya utafiti na maendeleo ya chanjo ambao wanafanya kazi pamoja kutengeneza chanjo dhidi ya magonjwa hatari ya kuambukiza.

Tarehe 7 mwezi huu wa February Taasisi ya afya ya Equatorial Guinea ilituma sampuli Kwenda kwenye maabara ya taasisi ya Pasteur nchini Senegal chini ya usaidizi wa WHO ili kubaini sababu ya ugonjwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa watudumu wa afya katika wilaya.

Katika sampuli nani zilizofanyiwa uchunguzi moja ilibainika kuwa na virusi vya ugonjwa huo.

Mpaka sasa kumeripotiwa vifo 9 na washukiwa 16 wa ugonjwa huo ambao wanaonesha dalili iliwemo kuchoka, kupata homa, kutapika na kuharisha damu.

Uchunguzi zaidi unaendelea ambapo timu za watalamu zimetumwa katika wilaya zinazoshukiwa kuwa na wagonjwa kwa ajili ya Kwenda kufanya uchunguzi.

WHO Afrika inafanya nini?

Juhudi pia zinaendelea ili kuongeza kasi ya kukabiliana na dharura hiyo ambapo WHO imetuma wataalam wake wa dharura katika magonjwa ya mlipuko, udhibiti wa wagonjwa, kuzuia maambukizi, maabara na mawasiliano ya hatari ili kusaidia juhudi za kitaifa za kukabiliana na kuhakikisha kuna usalama na ushirikiano na jamii katika kudhibiti milipuko.

WHO pia inawezesha usafirishaji wa hema zitakazotumika kama maabara kwa ajili ya uchunguzi wa sampuli pamoja na kifurushi kimoja cha homa ya virusi vya haemmorhagic ambacho kinajumuisha vifaa vya kujikinga ambavyo vinaweza kutumiwa na wahudumu 500 wa afya.

Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Dk Matshidiso Moeti, akizungumza kutoka Brazzaville nchini Kongo amesema “Marburg inaambukiza sana. Shukrani kwa hatua ya haraka na madhubuti kwa mamlaka ya Equatorial Guinea katika kuthibitisha ugonjwa huo, majibu ya dharura yanaweza kupatikana haraka ili kuokoa maisha na kukomesha virusi haraka iwezekanavyo."

Fahamu kuhusu ugonjwa wa Marburg

Ugonjwa wa virusi vya Marburg ni ugonjwa hatari sana unaosababisha homa ya kutokwa na damu, na uwiano wa vifo ni hadi asilimia 88.

Ugonjwa huu unaweka katika familia moja na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa virusi vya Ebola.

Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Marburg huanza ghafla, na homa kali, maumivu ya kichwa makali. Wagonjwa wengi hupata dalili kali za kuvuja damu ndani ya siku saba.

Virusi huingia kwa binadamu kutoka kwenye matunda yaliyoliwa na popo na huenea kati ya wanadamu kwa kuambukizana moja kwa moja kwa njia ya maji maji ambapo maambukizihutokea kwa kumshika aliyepata maambukizi, kushika maeneo aliyoshikana vitu alivyoshika.

Kuna chanjo ya Marburg?

Hakuna chanjo au matibabu ya ugonjwa huu. Hata hivyo huduma muhimu kama vile kurejesha maji mwilini kunywa maji kwa njia ya mdomo au ya mishipa na matibabu ya dalili maalum, yanasaidia kuokoa maisha.

Mpaka sasa bado hakuna takwimu kamili ila awamu ya kwanza ya takwimuinafanyiwa uchambuzi ambayo inahusisha matibabu mbalimbali kama vile watu kuwekewa damu, matibabu ya kinga na matibabu ya dawa, pamoja na watu kupatiwa chanjo.