Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa amani nchini DRC wasababisha watoto 750,000 kukosa elimu

Watoto wakimbizi wa ndani katika kambi moja iliyoko mjini Djugu jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
UN /Eskinder Debebe
Watoto wakimbizi wa ndani katika kambi moja iliyoko mjini Djugu jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Ukosefu wa amani nchini DRC wasababisha watoto 750,000 kukosa elimu

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataif linalohudumia watoto duniani UNICEF limesema nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC hali inazidi kuwa mbaya hali inayofanya elimu kwa watoto wapatao 750,000 kutatizika katika majimbo ya mashariki ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo kuwa takwimu mpya zilizotolewa na UNICEF zinaonesha kuwa kati ya mwezi Januari 2022 mpaka sasa, shule zisizopungua 2,100 katika mikoa 2 pekee zimelazimika kufunga milango yao kwa sababu ya hali ya usalama kuwa mbaya zaidi.

“Watoto waliyakimbia makazi yao kutokana na ghasia na hivyo kukatiza elimu yao.” alisema Dujarric

 Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa UNICEF ilisema ukubwa wa mzozo huo unamaanisha kwamba watoto wengi wanaoishi katika kambi za wakimbizi hawawezi kuwa na huduma zozote za elimu, na ni wachache tu kati ya watoto hao wanaoweza kufikia baadhi ya maeneo salama yaliyowekwa kwa ajili ya watoto yanayofadhiliwa na UNICEF au Vituo vya Kujifunza vya Muda.

Hata hivyo UNICEF inaendelea kusaidia ujenzi wa maeneo ya muda ya kujifunza na kutoa nyenzo za shule kwa wanafunzi, pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu kuhusu mada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.