Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Nilisikia sauti usiniache! ndipo nikakuta mtoto Anuarita"- Asema baba aliyenusuru mtoto msituni huko DRC

Anwarita akiwa nyumbani kwa wazazi wake walezi huko Bona, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
© UNICEF/Roger LeMoyne
Anwarita akiwa nyumbani kwa wazazi wake walezi huko Bona, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

"Nilisikia sauti usiniache! ndipo nikakuta mtoto Anuarita"- Asema baba aliyenusuru mtoto msituni huko DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Anwarita mtoto mwenye  umri wa miaka 8 amejikuta yatima baada ya waasi kuua kwa mapanga wazazi wake huko Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Hivi sasa Anwarita anaishi na familia iliyomnusuru msituni, wakati huu ambapo takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema kwa sasa watoto milioni 3 nchini humo wametawanyishwa na mizozo.
 

Dieudonne Aquatamba ni mkazi wa Boga jimboni Ituri na anasema, “nilikuwa niko shambani msituni, tarehe 19 mwezi Aprili mwaka 2020. Waasi wa ADF walishambulia. Tulikimbia lakini wakati nakimbia nasikia sauti yam toto analia, Usiniache! Usiniache! Usiniache!

Bwana Aquatamba ni baba wa familia akisimulia kisa cha kumuokoa mtoto Anwarita kutoka msituni anasema, “Niliposikia analia, nilifikiria, ingalikuwaje kama angalikuwa mtoto wangu? Ingawa waasi walikuwa wanaendelea kufyatua risasi, nilifikiria tena, siwezi kumuacha huyu mtoto, hivyo niliamua kurudi nyuma na kumuokoa!!”

Soundcloud

Wakiwa pamoja na Anwarita mwenye umri wa miaka minane, na watoto wengine wa Dieudonne kwenye makazi yao hapa Boga, Dieudonne anakumbuka alivyomkuta akisema, “nilipomuona, alikuwa amelala na alikuwa na jeraha kubwa mguuni. Walikuwa wamemshambulia kwa panga na waliua familia yake yote, waasi pia waliua watu wengi kwenye kijiji chao. Watu walikutwa wamekufa! Walichinjwa.”

Nilikuwa niko shambani msituni, tarehe 19 mwezi Aprili mwaka 2020. Waasi wa ADF walishambulia. Tulikimbia lakini wakati nakimbia nasikia sauti yam toto analia, Usiniache! Usiniache! Usiniache- Dieudonne Aquatamba,  Mkazi wa Ituri

Wakiwa katika kambi hii ya wakimbizi wa ndani Anwarita na nduguze wanakwenda kuteka maji ambapo Beatrice Casamira, mama mlezi wa Anwarita anasema, “namuona kama mwanangu wa kumzaa. Mume wangu alimleta hapa kutoka msituni na akaniambai, ‘lazima tumlee kama binti yetu’ kwa hiyo tunamlea kama binti yetu, na ni kama miongoni mwa binti zetu wa kuwazaa.”

Anwarita anasaidia kazi za nyumbani ambapo Beatrice anakumbuka hali ilivyokuwa pindi binti huyo alipowasili akisema, “mara ya kwanza alipofika hapa, kwa kweli ilikuwa vigumu mno. Niliona hali ambayo alikuwa nayo, na kwa siku mbili za mwanzo hakuweza kuzungumza chochote. Nilitambua kuwa amepata kiwewe mno. Lakini taratibu alianza kufunguka kwetu na kutusimulia yaliyomsibu. Bado ni mtoto mdogo, anapenda kucheza na watoto wengine, lakini pia anapenda kunisaidia jikoni.”

Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza katika kituo rafiki kwa watoto kambini Droro, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
© UNICEF/UN0377403/Roger LeMoyne
Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza katika kituo rafiki kwa watoto kambini Droro, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Anwarita anakoka moto na pia anasaidia kwenye maandalizi ya kupiga na kusonga ugali wa muhogo, halikadhalika kazi nyingine za nyumbani. Anwarita anasema, “Napenda kucheza na dada zangu na pia napenda kusaidia kazi za nyumbani. Napenda kuwepo hap ana wananitunza vyema na wananipenda.”

Chakula kimeiva na sasa ni wakati wa mlo familia nzima ikiwa imeketi pamoja, baba wa familia Dieudonne anasema, “sifahamu mustakabali wetu, lakini chochote kile kitakachotokea, tutamtunza kama binti yetu. Zaidi ya hayo Mungu anajua kilicho mbele yetu.”

Na kwa Beatrice, “kutokana na kile nilichokiona katika kipindi hiki amekuwa nasi, atakuwa sawa. Nadhani taratibu ataanza kurejea katika maisha ya kawaida. Pale ambapo watoto wengine wanauliza wazazi wake ni nani, yeye anaonesha nyumba yetu akisema mama na baba wanaishi pale. Kwa hiyo taratibu anaanza kutukubali kuwa sisi ni wazazi wake.”