Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili Kukabiliana na Ugaidi na Kuzuia Misimamo mikali ya Ghasia

Mwanajeshi kutoka Burkina Faso akiwa katika ulinzi kwenye mpaka wa Mali na Niger wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya washukiwa wa ugaidi.
© Michele Cattani
Mwanajeshi kutoka Burkina Faso akiwa katika ulinzi kwenye mpaka wa Mali na Niger wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya washukiwa wa ugaidi.

Baraza la Usalama lajadili Kukabiliana na Ugaidi na Kuzuia Misimamo mikali ya Ghasia

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameliambia Baraza la Usalama kwamba "anatiwa wasiwasi sana na mafanikio ambayo makundi ya kigaidi yanapata katika ukanda wa Sahel (barani Afrika) na kwingineko," akisisitiza kwamba "kama vile ugaidi unavyowatenganisha watu, kukabiliana nao kunaweza kuleta nchi mbalimbali pamoja." 

Baraza la Usalama leo (28 Machi) limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu "Kukabiliana na Ugaidi na Kuzuia Misimamo mikali ya Ghasia kwa Kuimarisha Ushirikiano Kati ya Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kikanda na Mbinu."

Guterres amesema kuwa ugaidi ndio mzizi na matokeo ya matatizo mengi yanayojadiliwa na Baraza hili la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hakuna umri, hakuna utamaduni, hakuna dini, hakuna utaifa na hakuna eneo ambalo lina kinga. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu tishio la kigaidi kwa amani na usalama kote ulimwenguni.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu tishio la kigaidi kwa amani na usalama kote ulimwenguni.

"Lakini hali barani Afrika inatia wasiwasi hasa, " Guterres ameonya. 

Bwana Guterres amesema kuwa kukata tamaa, umaskini, njaa, ukosefu wa huduma za kimsingi, ukosefu wa ajira, na mabadiliko yasiyo ya kikatiba serikalini yanaendelea kuweka msingi mzuri wa kupanuka kwa makundi ya kigaidi na kuambukiza maeneo mapya ya bara hilo. 

Hata hivyo, Guterres amesema Afrika pia ni nyumbani kwa mipango kadhaa ya kikanda ya kukabiliana na ugaidi, "kuanzia kwenye  juhudi za pamoja katika Sahel, Bonde la Ziwa Chad, Msumbiji na kwingineko. Kwa uamuzi mpya wa viongozi wa Afrika kukabiliana na tishio hili linaloendelea - kama inavyoonekana katika Mkutano wa hivi karibuni wa Umoja wa Afrika kuhusu ugaidi na mabadiliko ya serikali kinyume na katiba," Guterres ameeleza. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amerejelea kusema, "Umoja wa Mataifa unasimama na Afrika kukomesha janga hili." 

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza zaidi kuwa ni pamoja na mwongozo wa sera za Baraza la Usalama, usaidizi wa kiufundi na usaidizi wa vikwazo kwa tawala mbalimbali. Inajumuisha ziara 65 za tathmini za Kamati ya Kupambana na Ugaidi ili kuhakikisha utiifu wa mahitaji ya Baraza la Usalama - ambazo zilisababisha maelfu ya mapendekezo yanayoweza kutekelezwa kwa Nchi Wanachama kuboresha hatua za kuchukua. Inajumuisha kazi ya Umoja wa Mataifa kupitia Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Ugaidi kuleta pamoja mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, Nchi Wanachama, mabunge ya kikanda na mashirika ya kiraia ili kuunga mkono juhudi za pamoja katika bara zima. 

Zaidi ya yote, Guterres amesema kuwa ni pamoja na ushirikiano wa karibu unaoendelea wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika na mashirika ya kikanda ya Afrika. 

Aidha Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa ugaidi unawakilisha kunyimwa na kuharibu haki za binadamu. 

Amesema, "Ushahidi unaonesha kwamba juhudi za kupambana na ugaidi ambazo zinazingatia usalama pekee badala ya msingi wa haki za binadamu zinaweza kuongeza kutengwa na kufanya hali kuwa mbaya zaidi." 

Katibu Mkuu Guterres amehitimisha akisema, "Katika kila hatua, tunajitolea kudumisha haki muhimu na utu wa waathiriwa na manusura wa ugaidi kwa kusaidia na kusaidia kuponya wale ambao wamejeruhiwa na waliokimbia makazi yao." 

Azali Assoumani, Rais wa Comoro akizungumza kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika akihutubia baraza za usalama kuhusu tishio la kigaidi kwa amani na salama.
UN Photo/Eskinder Debebe
Azali Assoumani, Rais wa Comoro akizungumza kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika akihutubia baraza za usalama kuhusu tishio la kigaidi kwa amani na salama.

Azali Assoumani - Muungano waAfrika 

Kwa upande wake Azali Assoumani, Rais wa Comoro akizungumza kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika amesema, "kushirikiana habari muhimu, akili, uratibu wa shughuli zetu ni muhimu katika kuendeleza mafanikio yetu kama ilivyo ada kuzuia na kupambana na ugaidi na vitisho vingine vya mipakani." 

Rais Assoumani amehimiza Baraza la Usalama kuongeza maradufu juhudi zake na kuimarisha ushirikiano kati ya Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika kuzuia, “ni gharama ndogo katika muda mrefu." 

Ameongeza, "Mpango wa utekelezaji wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ugaidi na itikadi kali za kivita ungekuwa na athari kubwa kama ungepewa rasilimali zinazohitajika." 

Filipe Jacinto Nyusi 

Filipe Jacinto Nyusi, Rais wa Msumbiji pia amezungumza katika Baraza la usalama katika nafasi ya kiongozi wa taifa ambapo pia nchi yake inashikilia Urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Machi. 

Filipe Jacinto Nyusi, Rais wa Msumbiji pia amezungumza katika Baraza la usalama kuhusu tishio la kigaidi kwa amani na usalama kote ulimwenguni.
UN Photo/Manuel Elías
Filipe Jacinto Nyusi, Rais wa Msumbiji pia amezungumza katika Baraza la usalama kuhusu tishio la kigaidi kwa amani na usalama kote ulimwenguni.

"Kwa upande mmoja, itikadi kali kwa kuzingatia vigezo vya utambulisho vinavyochochewa na kutovumiliana, na kwa upande mwingine, udanganyifu wa mambo ya kijamii na kiuchumi umeongeza kasi ya uandikishaji kwa vikundi vya kigaidi, hasa vijana. Ushirikiano wa uhalifu wa kimataifa na uliopangwa wa magaidi umechangia kuishi na kuenea kwa vikundi vya kigaidi.” Amesema Rais Nyusi. 

Rais Nyusi pia ameongeza kusema, "Katika ngazi ya bara la Afrika, vikundi vya kigaidi vinafanya kazi na matukio mengi zaidi kaskazini mwa Afrika, Sahel, Afrika ya Kati, Pembe ya Afrika, Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika." 

Kiongozi huyo amerejelea kueleza kuwa Msumbiji inalengwa moja kwa moja na mashambulizi ya kigaidi tangu Oktoba 2017, na kuongeza kuwa "vitendo hivi vinasababisha vifo na uharibifu na kurudisha nyuma ajenda ya maendeleo kwa ajili ya ustawi wa watu wetu." 

Amani na Usalama 

Baraza la Usalama lina jukumu la msingi la kudumisha amani na usalama wa kimataifa. Lina Wajumbe 15, na kila Mwanachama ana kura moja. Chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Nchi zote Wanachama zina wajibu wa kuzingatia maamuzi ya Baraza. 

Baraza la Usalama linaongoza katika kuamua kuwepo kwa tishio dhidi ya amani au kitendo cha uchokozi. Linatoa wito kwa wahusika katika mzozo kusuluhisha kwa njia za amani na linapendekeza njia za kurekebisha au masharti ya suluhu. Katika baadhi ya matukio, Baraza la Usalama linaweza kuamua kuweka vikwazo au hata kuidhinisha matumizi ya nguvu kudumisha au kurejesha amani na usalama wa kimataifa.