Tunalaani tukio la Ugaidi nchini Kenya -Baraza la Usalama.

16 Januari 2019

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo mjini New York Marekani limelaani vikali shambulizi la kigaidi lililotekelezwa jana tarehe 15 Januari mjini Nairobi Kenya na kusababisha vifo vya watu 14 na majeruhi.

Kupitia taarifa yao waliyotoa leo, wanachama wa baraza hilo wameeleza masikitiko na kutuma salamu za rambirambi kwa waathirika na familia zao pamoja na watu wa Kenya na serikali yao. Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamewatakia ahueni ya haraka wale wote waliojeruhiwa.

Wanachama wa baraza hilo pia wametambua mchango wa Kenya katika mapambano dhidi ya ugaidi hususani mchango wa nchi hiyo katika vikosi vya muungano nchini Somalia (AMISOM) katika harakati za kupambana na Al-Shabaab.

Aidha wanachama wa Baraza la Usalama wamesisitiza umuhimu wa kuwafikisha katika vyombo vya haki wale wote waliohusika kwa njia moja au nyingine katika kupanga, kufadhili na kutekeleza matendo yasiyokubalika ya kigaid. 

Pia baraza hilo limeyasihi mataifa yote kwa mujibu wa sheria za kimataifa kushirikiana na serikali ya Kenya na mamlaka nyingine husika katika suala hilo.

Baraza la Usalama pia limesema matendo ya kigaidi ni uhalifu na hayakubaliki bila kujali mwanachokipigania magaidi, popote na yeyote anayehusika.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter