Baraza la Usalama lapitisha azimio la aina yake la kupinga ufadhili wa ugaidi

Baraza la Usalama wakati wa kikao cha kujadili tihsio dhidi ya usalama kimataifa unaosababishwa na vitendo vya kigaidi uliofanyika Machi 28, 2019, New York.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Baraza la Usalama wakati wa kikao cha kujadili tihsio dhidi ya usalama kimataifa unaosababishwa na vitendo vya kigaidi uliofanyika Machi 28, 2019, New York.

Baraza la Usalama lapitisha azimio la aina yake la kupinga ufadhili wa ugaidi

Amani na Usalama

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la aina yake ambalo linazuia ufadhili wa vikundi vya kigaidi kote ulimwenguni.

Akihutubia baraza hilo kwa njia ya video kutoka Roma, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na masuala ya ugaidi, Vladmir Voronkov amesema kupitishwa kwa azimio hilo kumefanyika wakati muafaka, wakati huu ambapo mashambulizi ya hivi majuzi yameonyesha kwamba makundi ya kigaidi yana raslimali halali na zisizo halali za kupata fedha.

Bwana Voronkov akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kwa ajili ya juhudi za pamoja ili kufikia matokeo thabiti katika vita dhidi ya ugaidi na ufadhili wa ugaidi amesema azimio namba 2462 kuhusu kukabiliana na ufadhili wa ugaidi, linazingatia maazimio mengine kwa ajili ya kuunda nyaraka moja ambayo pia inashughulikia changamoto zinazojitokeza.

Azimio hilo linaitaka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi iliyoanzishwa mwaka 2017 kuimarisha uwezo wake wa kutekeleza mkakati wa kimataifa wa kukabiliana na ugaidi kwa kuchukua uongozi wa jinsi ya kukabiliana na ufadhili wa ugaidi.

Bwana Voronkov amesema ni kwa kupitia ushirikiano wa hali ya juu tu na juhudi za pamoja, ndiko kutakakoleta matokeo chanya katika vita dhidi ya ufadhili wa ugaidi.

Katika hotuba yake hiyo kwa baraza la usalama, bwana Voronkov ametaja vipaumbele vitatu, mosi kupanua wigo wa kazi za ofisi ya kukabiliana na ugaidi kuhusisha na pia kubadilishana  taarifa za kiintelejensia, na kutathmini hatari na ushirikiano wa umma na binafsi. Pili kuweka mfumo wa kujenga uelewa na kubuni njia ya kukabiliana na changamoto, na tatu kufanya kazi karibu na shirika la kimatiafa la kufuatilia fedha ambalo linaweka vipimo vya kukabiliana na utakatishaji wa fedha, ufadhili wa magaidi na matishio mengine yanazohusiana na utendaji wa mifumo ya fedha na wasimamizi wa kikanda.

Marshall Billingslea, rais wa shirika la kimatiafa la kufuatilia fedha amehutubia pia kikao hicho na kukaribisha hatua kwamba azimio linatoa wito kwa mataida kufanya mengi zaidi kuzuia malipo ya fidia kwa magaidi ambayoa alisema inawachochea kuendelea kuteka kama mbinu ya kujipatia kipato. Aidha amezingatia kwamba kwa sasa mataifa theluthi mbili hayashtaki wafadhili wa ugaidi ambao unakwenda zaidi ya sekta ya benki na fedha na kujumuisha ujenzi, usafirishaji wa mihadarati na hata biashara ya magari.

Kwa upande wake Mercy Baku mtaalam wa kukabiliana na ufadhili wa ugaidi akizungumza kwa njia ya video kutoka Nairobi Kenya amesema matokeo ya mashambulizi ya hivi karibuni ya kigaidi bado yapo akilini mwa raia na akapongeza azimio hilo kama la wakati muafaka katika kuchagiza vita dhidi ya ugaidi, ufadhili wa magaidi na utakatishaji wa fedha huku akitoa angalizo kwamba vita dhidi ya ugaidi visiingilie mikakati ya kujumuisha wote kifedha ambazo zinawezesha waktu kupata huduma za benki nza zenye lengo la kupunugza umasikini na ukosefu wa usawa.