Watu zaidi ya watu 128 wauawa kigaidi Pakistan, UN yalaani vikali

14 Julai 2018

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shmbulio la kigaidi mjini Mastung, Pakistan lililotokea Ijumaa 13 Julai, na kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 128 na wengine 200 kujeruhiwa.

Wajumbe wa baraza hilo wametuma salam za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha, watu na serikali ya Pakistan na kuwatakia ahuweni ya haraka wote waliojeruhiwa.

Wajumbe hao wamerejea kauli yao kwamba, ugaidi katika mfumo wowote ule ni moja ya tishio kubwa kabisa la amani na usalama wa kimataifa na kusisitiza haja ya kuwafikisha kwenye mkono wa sheria wote waliohusika na ukatili huo , iwe ni waandaaji, wafadhili na wawezeshaji, na kuzitaka nchi zote kutekeleza wajibu wao wa kimataifa na kwa kuzingatia maazimio ya Baraza la Usalama na kushirikiana kikamilifu na serikali ya Pakistan na wadau wengine katika suala hili.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza tena kwamba vitendo vyovyote vya kigaidi ni kosa la jinai na lisilohalalishwa kwa namna yoyote ile, bila kujali lengo, wapi, wakati gani na nani aliyetekeleza.

Wamehimiza haja ya mataifa yote kupambana na ugaidi kwa kila njia , kwa kuzingatia katiba ya Umoja wa Mataifa na wajibu chini ya sheria za kimataifa, zikiwemo sheria za kimataifa za haki za binadamu, haki za kimataifa za wakimbizi, haki za kimataifa za masualaya kibinadamu na tishio kwa amani na usalama wa kimataifa linaloletwa na vitendo vya kigaidi.
TAGS: Baraza la Usalama, Pakistan, Ugaidi, 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter