Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila mazingira na sera madhubuti, nchi maskini kutonufaika na teknolojia rafiki kwa mazingira- UNCTAD

Kinyozi huyu nchini Malawi anatumia paneli hii ya sola aliyopatiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO nchini humo.sola kwa ajili ya kazi yake.
ILO/Marcel Crozet
Kinyozi huyu nchini Malawi anatumia paneli hii ya sola aliyopatiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO nchini humo.sola kwa ajili ya kazi yake.

Bila mazingira na sera madhubuti, nchi maskini kutonufaika na teknolojia rafiki kwa mazingira- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Teknolojia rafiki kwa mazingira ambazo hutumika kuzalisha huduma na bidhaa lakini kwa kutoa kiwango kidogo cha hewa chafuzi zinazidi kushamiri kila uchao na kupanua fursa za kiuchumi, lakini nchi nyingi maskini ziko hatarini kuzikoka iwapo serikali na jamii ya kimataifa hawatachukua hatua madhubuti.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo ya biashara duniani, UNCTAD ikipatiwa jina Ripoti ya Teknolojia na Ubunifu ya mwaka 2023.

Ripoti hiyo inaonya kuwa ukosefu wa usawa kiuchumi unazidi kuongezeka kwa kuwa nchi zilizoendelea zinanufaika zaidi na teknolojia zisizoharibu mazingira kama vile akili bandia, intaneti na magari yanayotumia nishati ya umeme.

"Ndio kwanzo tuko mwanzoni kabisa mwa mapinduzi ya kiteknolojia yanayotumia nishati rafiki kwa mazingira,” amesema Rebeca Grynspan Katibu Mkuu wa UNCTAD akinukuliwa kwenye taarifa iliyotolewa ikichambua ripoti hiyo huku akisema “wimbi jipya la teknolojia litakuwa na mabadiliko makubwa kwenye uchumi wa dunia. Nchi zinazoendelea zinapaswa kuvuna zaidi thamani itokanayo na mapinduzi haya ili zikuze uchumi wao.”

Mkuu huyo wa UNCTAD amesema kukosa kunufaika na wimbi hili kwa sababu ya ukosefu wa sera madhubuti na sahihi au kwa kukosa uwekezaji katika kujenga uwezo kutakuwa na madhara ya muda mrefu.

Soko linakua huku pengo la teknolojia likipanuka

UNCTAD inakadiria kuwa aina 17 za teknolojia za kisasa zilizotajwa kwenye ripoti hiyo zinaweza kupanua soko lenye thamani ya dola trilioni 9.5 ifikapo mwaka 2030, kiwango ambacho ni mara tatu zaidi ya ukubwa wa thamani ya uchumi wa India.

Hata hivyo ripoti inasema kwa sasa ni nchi tajiri pekee ndio zinanufaika na fursa hizo huku nchi maskini zikiachwa nyuma.

Thamani ya jumla ya teknolojia rafiki kwa mazingira ambazo ziliuzwa nje kutoka nchi zilizoendelea iliongezeka kutoka dola bilioni 60 mwaka 2018 hadi zaidi yad ola bilioni 156 mwaka 2021.

Tweet URL

Na katika kipindi hicho hicho mauzo ya teknolojia hizo kutoka nchi zinazoendelea au maskini yaliongezeka kutoka dola bilioni 57 hadi dola bilioni 75 pekee.

Katika kipindi cha miaka mitatu kiwango cha mauzo ya bidhaa kutoka nchi zilizoendelea kilishuka kutoka asilimia 48 hadi asilimia 33.

Ni kwa mantiki hioy uchambuzi wa UNCTAD unaonesha kuwa nchi zinazoendelea lazima zichukue hatua haraka ili kunufaika na fursa ya sasa ya teknolojia rafiki na kuwa na mipango ya maendeleo inayofungua fursa ya uchumi unaotegemea vyanzo mbali mbali.

Mapinduzi ya awali ya teknolojia yalidhihirisha kuwa wale wanaopiga hatua haraka na kutumia ndio wanakuwa na faida za muda mrefu.

Teknolojia hizo za kisasa na rafiki kwa mazingira ni zipi?

Kando mwa teknolojia za kisasa na rafiki kwa mazingira, ziko zile nyingine za kisasa kama vile matumizi ya ndege zisizo na rubani na uhariri wa kijenetiki.

Teknolojia hizo pamoja na magari yanayotumia nishati ya umeme, nishati ya sola na nishati ya upepo zinatarajiwa kufikia thamani ya dola trilioni 2.1 mwaka 2030, ikiwa ni mara nne zaidi ya thamani zao hii leo.

Mapato yatokanayo na magari yanayotumia nishati ya umeme yanaweza kuongezeka mara tano zaidi na kuwa thamani ya dola bilioni 824 mwaka 2030 kutoka thamani ya sasa ya dola bilioni 163.

Nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara safari bado ndefu

Ripoti imezipanga nchi 166 kwa kuzingatia vigezo vya TEHAMA, stadi, tafiti na maendeleo, uwezo wake kiviwanda na ufadhili wa fedha.

Kipimo hicho kinashikiliwa zaidi na Marekani, Sweden, Singapore, Uswisi na Uholanzi.

Ingawa nchi zinazoendelea hazijajiandaa vya kutosha kutumia teknolojia za kisasa, baadhi yao kama barani Asia zimefanya mabadiliko ya kisera ya kuziwezesha kuinuka zaidi tofauti na ilivyotarajiwa.

India inasalia kushika nafasi ya juu kwenye kipimo hicho ikishika nafasi ya 67 huku Ufilipino ikiwa ya 54 na Vietnam ya 44.

Nchi za Amerika Kusini, Karibea na Afrika kusini mwa jangwa la Sahara bado hazijajiandaa kunufaika na teknolojia za kisasa na ziko hatarini kukosa fursa ya sasa.

Jawabu ni sera za kijasiri za ndani na za nje

UNCTAD inasema hatua za kijasiri za serikali zinahitajika na hivyo zinapaswa kutunga será sahihi.

Halikadhalika ushirikiano wa kimataifa nao unatakiwa kwani kutunga será za ndani pekee bila kujumuisha na za kimataifa kupitia biashara ya kimataifa haitaleta mabadiliko.

“Kanuni za kimataifa za biashara zinapaswa kuruhusu nchi zinazoendelea kulinda viwanda vinavyoibuka vinavyotumia teknolojia rafiki kwa mazingira, kanuni kama vile ushuru, ruzuku na manunuzi ya umma,” imesema ripoti hiyo.