Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia mpya zina hatari kubwa:Boris Johnson

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la UN
Picha ya UN/ Cia Pak
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la UN

Teknolojia mpya zina hatari kubwa:Boris Johnson

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Teknolojia mpya zina hatari kubwa, ameonya waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akihutubia Jumanne usiku mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York Marekani.

Hata hivyo waziri Mkuu huyo amesema nchi yake ya Uingereza iko mstari wa mbele katika kulinda intelejensia ya teknolojia ya kidijitali.

Boris Johnson aliyeshika hatamu kama Waziri Mkuu wa serikali ya kifalme ya Uingereza mwezi Julai mwaka huu amewakaribisha wajumbe wa mkutano wa Baraza Kuu kwenda London ambako mwakani ataitisha mkutano wa kimataifa kuhusu masuala hayo ya teknolojia mpya.

Akijinasibu kuhusu uwezo wa taifa lake amesema “tuna sekta ya teknolojia iliyo piga hatua kubwa sana , ama iwe teknolojia ya nano au teknolojia inayojali mazingira au hata teknolojia mpya kabisa.”

Kwa mujibu wa Johnson hakuna nchi yeyote inayopaswa kutoshirikishwa kwenye teknolojia hizi au kutengwa . Ametoa wito wa wa kuwepo na uwiano baina ya uhuru wa kuunda na uhuru wa kutumia teknolojia hizi , baina ya udhibiti wa serikali na uhuru wa faragha.

Akifafanua kuhusu mkutano ujao mjini London waziri mkuu ameonya kwamba “ Hatuwezi kupuuza nguvu ya mabadiliko, leo hii unaweza kuficha vitu wasivione marafiki zako, wazazi wako, Watoto wako na hata Daktari wako lakini huwezi kuficha kwa Google. Teknolojia inaweza kutumika kumfuatia kila raia kwa saa 24 kwa siku na kesho jokofu lako litaweza kukuamlia mlo unaokufaa.”

Ameongeza kuwa kimbunga kitalipuka na hatujui jinsi ya kukidhibiti. "Hatujui nani atakayetumia rasilimali na yanayojiri , hatujui kama mashine hizo zimetengenezwa ili kutudanganya , ukizingatia kwamba katika baadhi ya visa udikteta wa kidijitali uko bayana. Na hii inaweka mustakbali wa kila mmoja njiapanda,"  amesema waziri Mkuu huyo wa Uingereza.