Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya umeme wa Sola yawezesha huduma za mahakama kupatikana muda wote nchini Kenya

Wanaume wawili wakipakia paneli za jua kwenye boti ndogo katika Ziwa Turkana nchini Kenya.
Climate Visuals Countdown/Maurizio Di Pietro
Wanaume wawili wakipakia paneli za jua kwenye boti ndogo katika Ziwa Turkana nchini Kenya.

Matumizi ya umeme wa Sola yawezesha huduma za mahakama kupatikana muda wote nchini Kenya

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na madawa ya kulevya na uhalifu UNDOC kanda ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na sekta ya mahakama nchini kenya wamepanga kuanza kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa uwekaji umeme wa sola katika mahakama na magereza nchini humo baada ya awamu ya kwanza kuonesha mafanikio.

Kupitia mradi ujulikanao kama PLEAD unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya, EU, UNODC na sekta ya mahakama nchini Kenya wamefanikiwa kutekeleza mradi wa awamu ya kwanza katika mahakama mbili zilizoko Mombasa ambazo zilikuwa zikishindwa kuendesha shughuli zake pindi umeme unapokatika.

Francis Kilonji Jackson, mfanyakazi wa mahakama ya watoto ya Tononoka iliyoko Mombasa anaeleza kuhusu tatizo la umeme kukatika. “Unajua kumuelezea mtu kwaba hatumwezi kukuhudumia sababu hatuna umeme ilikuwa ni shughuli kubwa, mtu ametumia hela yake ya nauli kutoka mbali kama Kaunti ya Kwale, Kilifi, au mbali huko Taita Tavera kuja hapa Mombasa kwenye mahakama hii kupata huduma alafu anakuta hatuna umeme na hatuwezi kumuhudumia tunampa tarehe nyingine aje ndio tuweze kumuhudumia tulikuwa tunachanganyikwa kabisa.”

Ili kuondokana na changamoto hii mradi wa PLEAD ukaanzishwa katika mahakama mbili, ya watoto ya Tononoka na Shanzu na mshauri Mkuu wa Uhandishi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC Bernard Odhuno anaeleza mchakato wake.

“Tungeweza kuchagua kutumia genereta katika kukabiliana na changamoto hii lakini katika mazungumzo yetu na mfadhili tuliona ni vyema sisi kuwa waanzilishi wa mradi ambao ni rafiki kwa mazingira”

Mhandisi Bernard anaendelea kwakufafanua suala la gharama kubwa ya uwekaji wa sola.

“Nishati hii kwanza ni salama, pili ni ya uhakika, na tatu inajitosheleza kwa malighafi na gharama. Ni kweli gharama ya uwekezaji wa mradi inaweza kuwa kubwa lakini gharama za uendeshaji zitaendelea kupungua na kufidia gharama kubwa za mtaji zilizowekezwa na kusaidia sana katika utoaji wa haki kwa mwananchi.”

Mfumo wa umeme wa Sola uliofungwa katika mradi huu wa PLEAD unaweza kutoa huduma kwa takriban siku tano na Mohammed Adan Abdi afisa utawala katika mahakama ya Shanzu anasema sasa kazi zinaenda vyema.

“Tukipoteza umeme wa kawaida unaosambazwa na serikali, umeme wa nguvu ya Sola unafanya kazi kwani umeunganishwa moja kwa moja ule ukikatika huu wa Sola unawake, hii inamaana utoaji wa huduma haitasimama. Sekta ya mahakama imekumbatia teknolojia ili kuwezesha utoaji wa haki, ulipaji faini za makosa mbalimbali, kulipa fedha kwa ajili ya dhamana na vitu kama hivyo vyote sasa vinafanyika kwenye mfumo, hivyo bila umeme kazi zote hizo zinasimama.”

Awamu ya pili ya mradi

Baada ya awamu ya kwanza kuonesha mafanikio, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na madawa na uhalifu UNODC kanda ya Afrika Mashariki Charity Kangwi- Ndung’u anasema sasa wanajipanga kuanza utekelezaji wa awamu ya pili mapema mwaka 2023.

“Katika awamu yetu ya miaka 5 tumeona ni dhahiri wanatafuta njia endelevu ya kufanya biashara, yenye kujali mazingira na wanataka kuongeza maeneo mengine ili kudhihirisha kuwa kutumia umeme wa sola ni jambo linawezekana kufanyika.”

Katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo jumla ya vituo 9 vinategemea kunufaika na umeme wa nishati ya jua. Vituo hivyo ni Mahakama ya Winam, Maseno, Garsen, Shanzu na mahakama ya watoto wa Tokonono, Wajir, Isiolo, Madaraka pamoja na mahakama ya Kibera.

Mradi huo unategemewa kuboresha miundombinu katika vituo vya mahakama na magereza yaliyochaguliwa, hasa kwa kuweka nishati ya jua ili kuhakikisha kuna upatikanaji unaoaminiwa wa nishati na mtandao, huku kukiwa na utunzaji wa mazingira.