Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Soma Bag: Mabegi ya mgongoni yanayotumia sola mkombozi kwa wanafunzi

Begi la sola lililotengenezwa kwa kutumia taka mali. Kipande cha sola kimeunganishwa na waya inayopokea nishati ya jua na kuingiza katika taa maalumu ambayo usiku hutumika kwa ajili ya kujisomea
UN News
Begi la sola lililotengenezwa kwa kutumia taka mali. Kipande cha sola kimeunganishwa na waya inayopokea nishati ya jua na kuingiza katika taa maalumu ambayo usiku hutumika kwa ajili ya kujisomea

Soma Bag: Mabegi ya mgongoni yanayotumia sola mkombozi kwa wanafunzi

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Lengo namba nne la Malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs linazungumzia juu ya elimu bora, yenye usawa na kutoa fursa kwa wote, na hicho ndicho kinachofanyika jijini Mwanza kaskazini Magharibi mwa Tanzania ambapo vijana wamebuni mradi wa mabegi yanayokusanya nishati ya jua ili kuwasaidia wanafunzi waishio vijijini kujisomea nyakati za usiku.

Ubunifu wa mradi huu wa mabegi uliopewa jina la Soma Bag unaenda kutibu kiu ya Wanafunzi wengi hususani wanaoishi maeneo ya vijijini nchini Tanzania ambao wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya kujisomea nyakati za usiku hatua ambayo huwalazimu kutumia kibatari ama taa za chemli ili kupata mwanga wa kujisomea.

Kusoma kwa kwa kutumia kibatari ama taa za chemli hutajwa kuwa ni kikwazo katika ufaulu wa wanafunzi kutokana na kuhitaji kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kununulia mafuta ya taa ambayo hutumika kuwashia nishati hiyo.

Muasisi wa Mradi wa Soma Bag Innocent Joseph,akionesha taa ambayo huchajiwa na solar punde mwanafunzi anapokuwa amevaa begi
UN News
Muasisi wa Mradi wa Soma Bag Innocent Joseph,akionesha taa ambayo huchajiwa na solar punde mwanafunzi anapokuwa amevaa begi

Wazo lilipoanzia

Katika mahojiano maalum aliyofanyiwa na Evarist Mapesa wa redio washirika wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa SAUT FM iliyoko mkoani Mwanza Tanzania, Innocent James ambaye ni muasisi wa mradi huo, anasema wazo lilianza pale walipokuwa wakijaribu kutatua changamoto ya wanafunzi kujifunza wenyewe na kuanza kuwajengea tabia ya kujisomea wenyewe kwa kuanzisha maktaba tembezi ambayo ilikuwa ikiwafuata watoto mahali wapo kama mashuleni au uwanjani.

Huduma hiyo ilianza kukuwa, huku wakijiuliza maswali, wanafunzi wangapi wanaitumia huduma hiyo? na inawafaa vipi katika masomo na ufaulu wao?. Walipofanya utafiti wakagundua Watoto waliokuwa wakichukua vitabu katika maabara tembezi hawakuvisoma ipasavyo.

Na miongoni mwa sababu walizozigundua kwa watoto hao kutosoma vitabu walivyokuwa wakivichukua ni kutokuwa na nishati rafiki ya kuwasaidia kujisomea nyakati za usiku.

“Tuligundua kwamba watoto wanapokuwa nyumbani nyakati za usiku wanawasha kibatari ambacho kinatumia mafuta ya taa, na kwa kawaida hakitoi mwanga wa kutosha wa kumvutia kusoma, pili unazalisha moshi ambao kimsingi unaleta kero kwa mtumiaji, na tatu ni gharama kununua mafuta hayo. Hapo ndipo tuliweza kubuni mabegi haya ili kuwasaidia wanafunzi kujisomea nyakati za usiku”, alisema James.

Kwa sasa James na wenzake wana kiwanda cha kutengeneza bidhaa hiyo, kwa siku huzalisha zaidi ya mabegi 100 ambayo huyauza na kuyasambaza katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania.

Taka mali ikiwa ipo katika hatua za utengenezwaji wa begi za wanafunzi. hatua inayofuata ni uunganishaji wa mikandazipukipande cha sola pamoja na waya
UN News
Taka mali ikiwa ipo katika hatua za utengenezwaji wa begi za wanafunzi. hatua inayofuata ni uunganishaji wa mikandazipukipande cha sola pamoja na waya

Mabegi hayo ni mkombozi wa mazingira

Mabegi hayo mbali na kusaidia wanafunzi lakini pia ni rafiki wa mazingira kutokana na malighafi yanayotumika kuwa ni taka mali za aina mbalimbali.

“Begi zetu tunatengeneza kwa kutumia mifuko ambayo inatumika kama vifungashio, hivyo huwa tunachukua mifuko hiyo ambayo inakuwa imeisha matumizi yake kama saruji na mifuko ya unga wa kufulia nguo tunazikusanya kwa pamoja”

Kutokana na kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira na viumbe hai vilivyopo aridhini, wameanzisha mfumo wa uchakataji wa maji (water recycle system) ambao huwawezesha kutumia maji wanayooshea mifuko ya saruji na kisha kuyatumia tena katika shughuli nyingine bila kuathiri mazingira.

Maji hayo hupitia katika hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na sehemu ambayo mifuko huoshewa, kisha hupelekwa katika hatua ya pili ambayo ni ya usuuzaji wa mifuko, kisha hubadilika kuwa maji taka, na baadae hupitishwa katika chujio maalumu na kuzalisha maji safi ambayo hurudi tena katika hali yake ya kawaida.

“Kutokana na kwamba sisi tunatumia zaidi mifuko ya saruji, na kama unavyojua kuwa saluji ina kemikali, na katika kila mfuko wa kuna mabaki kidogo yanayobaki kwenye mfuko, kwahiyo sisi tunavyoichukua na kufanya uoshaji mabaki hayo huchanganyikana na maji na yanapochanganyikana na maji huwa ni maji taka hayafai tena kwa matumizi ya kawaida”.

Anaendelea na kueleza mchakato huo “Hivyo inatulazimu kuyamwaga yale maji ambayo yanakwenda kwenye udongo, kwakweli hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa kwasababu kwa mwezi tunaweza kuwa na mabaki mengi ya saruji na kama tukiyaachia maji hayo yakaenda kwenye udongo yanaweza kuleta madhara kwenye mimea, udongo wenyewe au viumbe vingine vinavyoishi chini ya ardhi”.

Kwa mwezi mmoja hukusanya udongo wa saruji tani mbili uliopatikana katika mifuko wanayotumia ambayo huikusanya kwa ajili ya kutengeneza mabegi yanaenda kuwasaidia wanafunzi waishio vijijini nchini Tanzania.

Begi hilo linakusanyaje nishati ya jua?

Begi hili ambalo hutengenezwa kwa taka mali ikiwemo mifuko ya saluji ambayo hukusanywa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kisha husafishwa na kuunganisha kipande cha kifaa kinachonasa nishati ya jua (Sola).

Nishati hiyo hukusanywa kwa siku nzima kwani kipande hicho cha Solar kinakuwa kimeshonwa nyuma ya begi la mwanafunzi, ndani ya begi kunakuwa na taa ya kutoa nishati ya mwanga (bulb) ambayo inakuwa imeunganishwa na waya unaotoka kwenye sola.

Hivyo nyakati za usiku mwanafunzi anapokuwa anataka kusoma, huchomoa taa hiyo na kuiweka sehemu yeyote anayohisi akiiweka taa hiyo itampa mwanga mzuri wa kumuwezesha yeye kusoma vizuri bila usumbufu wowote.

UN News video/Evarist Mapesa
UN News
UN News video/Evarist Mapesa

Wanafunzi wafurahi

Soundcloud

Baadhi ya kaya hususani zilizoko katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania hazijafikiwa na huduma ya umeme hivyo hulazimika kutumia nishati mbadala na wengine kutumia vibatari na taa za chemli.

Wanafunzi wanaosoma shule za upili hususani wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania wamekuwa wakilazimika kutumia taa za chemli na vibatari ili kupata mwanga wa kujisomea, lakini ujio wa mabegi hayo, yameanza kuleta matokeo chanya katika ufaulu wa darasani.

Janeth Andrea ni mwanafunzi wa darasa la sita, anakiri kuwa uwepo wa mabegi hayo umemsaidia katika usomaji hasa nyakati za usiku.

Kwa upande wake Jackline Andrea anasema “taa hunisaidia usiku, zamani nilikuwa nasoma na taa ya nyumbani, ilikuwa na mwanga mdogo lakini taa hii ya begi ina mwanga mkali”

Wazazi wafurahia taa hizo

Andrea Busabusa ni mzazi wa Watoto wawili ambao wanatumia mabegi hayo yanayokusanya mwanga wa jua, anasema yamewasaidia Watoto wake hasa katika maendeleo ya ufaulu shuleni.

“Maendeleo ni mazuri, kwa watoto wangu wawili mmoja anakuwa wa nnee mwingine wa tano, ni kiwango kizuri kabisa kwasababu akiwa shuleni anaona kwa macho kwa kutumia mwanga wa jua, akirudi nyumbani anasoma kwa kutumia mwanga wa sola muda wowote anaoutaka”

Taa hizi iwapo zitasambazwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania zitaenda kuwasaidia wanafunzi hususani wale waishio maeneo ya vijijini kujisomea vizuri nyakati za usiku na hatimaye kutimiza malengo yao.