Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika tumieni fursa ya biashara huru kukuza viwanda na uchumi:UNIDO

Tanzania imeshuhudia kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi lakini kutokuwepo usawa hususani miongoni mwa wanawake imesalia kuwa changamoto
Picha na UNCTAD
Tanzania imeshuhudia kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi lakini kutokuwepo usawa hususani miongoni mwa wanawake imesalia kuwa changamoto

Afrika tumieni fursa ya biashara huru kukuza viwanda na uchumi:UNIDO

Ukuaji wa Kiuchumi

Katika miongo michache ijayo Afrika imeelezwa itakuwa bara changa na lenye watu wengi zaidi duniani , huku idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi ikitarajiwa kuongezeka na kufikia milioni 450 sawa na asilimia 70 ifikapo mwaka 2030.

Hayo ni kwa mujibu wa makadirio yaliyotolewa leo na  shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO wakati wa mjadala wa wazi wa Baraza Kuu uliobeba kaulimbiu,  " Kuimarisha ushirika wa kimataifa kwa ajili ya muongo wa maendeleo kwa ajili ya Afrika IDDA," kama chachu ya mafanikio ya utekelezaji wa eneo huru la biashara Afrika (AfCFTA).

Akizungumza katika ufunguzi wa mjadala huo mkurugenzi mkuu wa UNIDO Li Yong amesema mjadala wa leo umejikita katika mada kuu mbili , mosi kukumbatia awamu mpya ya biashara Afrika:changamoto na fursa kwa ajili ya ukuaji wa viwanda Afrika, na pili “kuimarisha ushiriki wa jumuiya ya kimataifa katika maendeleo ya viwanda barani Afrika hasa baada ya uzinduzi wa eneo la biashara huru barani humo.

Ameongeza kuwa tangu kuanza kwa karne hii Afrika imeshuhudia ukuaji wa uchumi , hata hivyo umasikini unaendelea kwa watu wa bara hilo hususan Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku ukosefu wa ajira na kutokuwepo usawa vikisalia juu.

UNIDO inasema watu wa vijijini na watu masikini mijini , wanawake na vijana hawajafaidika na ukuaji huo wa uchumi.

Hivyo watunga será wa Afrika wamebaini kwamba ili faida ya ukuaji uchumi iwe kwa wote ni lazima kuwe na mabadiliko ya mundo wa uchumi.

Hata hivyo shirika hilo limeongeza kuwa Afrika ina fursa kubwa ya kupunguza umasikini na kutokuwepo usawa na kuongeza fursa za ajira kwa vijana kwani AfCFTA inao uwezo wa kuwa biashara kubwa kabisa huru duniani ikiwa na soko la watu bilioni 1.2 ambao kwa pamoja watafanya pato la taifa kuwa zaidi ya dola trilioni 3.5.

Pia UNIDO imewaeleza washiriki wa mjadala huohuo kuwa biashara miongoni mwa nchi za Afrika itazisaidia nchi hizo kupanua wigo wa uchumi, ukuaji wa viwanda na kuongeza ajira na kipato kwa watu wake huku biashara huru ikiliondoa bara hilo kutoka kuwa tegemezi wa rasilimali na kuingia katika ushindani wa biashara yenye tija kwa uchumi.

Mkutano huo ambao umehutubiwa pia na naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed na Rais wa Rwanda Paul Kagame kama mwenyekiti wa sasa wa Muungano wa Afrika umewaleta pamoja wadau zaidi ya 100 wakiwemo wakuu wa nchi na wawakilishi, wawakilishi wa jumuiya za kiuchumi za bara la Afrika, taasisi za fedha, mashirika ya Umoja wa Mataifa, washirika wa maendeleo na uchumi, asasi za kiraia na wanazuoni.

Mjadala huo umeandaliwa kwa pamoja na UNIDO, Muungano wa Afrika AU na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO.