Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa ILO ameonya juu ya kuongezeka kwa pengo la usawa duniani, akitaka kutendeka haki ya kijamii

Mwanaume akifanyakazi kiwandani jijini Dar es salaam Tanzania
© ILO/Marcel Crozet
Mwanaume akifanyakazi kiwandani jijini Dar es salaam Tanzania

Mkuu wa ILO ameonya juu ya kuongezeka kwa pengo la usawa duniani, akitaka kutendeka haki ya kijamii

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kazi la Umoja wa Mataifa ILO, Gilbert F. Houngbo, ameonya kuhusu ongezeko la ukosefu wa usawa duniani kote, unaohusishwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei, kupanda kwa gharama za maisha, ongezeko la umaskini, na mgogoro wa madeni katika nchi zakipato cha chini na cha kati

Akizungumza katika kikao cha ufunguzi cha dodi ya  uongozi ya ILO, Houngbo amesema “hili lilithibitisha hitaji la dharura la kuzindua muungano wa kimataifa wa haki ya kijamii na kukabiliana na ukosefu wa usawa wa kiuchumi na kijamii.”

Muungano wa kimataifa ni jawabu mujarabu

Muungano wa kimataifa ni mojawapo ya masuala kadhaa muhimu ya ulimwengu wa kazi kwenye ajenda ya kikao cha 347 cha bodi ya uongozi ya ILO, ambacho kinahudhuriwa na wawakilishi wa Serikali, wawakilishi wa wafanyakazi na wawakilishi wa waajiri.

Muuguzi akimlisha mtoto mchanga chakula kwa njia ya mpira kwenye wadi ya watoto wachanga katika hospitali ya Muhima iliyoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
© UNICEF/Veronica Houser
Muuguzi akimlisha mtoto mchanga chakula kwa njia ya mpira kwenye wadi ya watoto wachanga katika hospitali ya Muhima iliyoko mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Pamoja na mapendekezo ya kuanzishwa kwa muungano huo mwezi Juni, baraza linaloongoza ILO litajadili hali ya Ukraine inayotokana na uvamizi wa Urusi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, mkurugenzi mkuu amesema ILO inapanga kupanua ofisi yake huko Kyiv na kuongeza msaada kwa Ukraine, nchi jirani kama Moldova, na maeneo mengine yaliyoathiriwa na vita.

Wakati wa mkutano wake, bodi pia itapokea ripoti ya mkurugenzi mkuu, kukagua kesi kadhaa za nchi ambazo ziko chini ya utaratibu wa malalamiko wa ILO, kufanya majadiliano kuhusu ugavi na uchumi wa jukwaa la kidijitali, na kuchunguza mapendekezo ya mpango na bajeti ya 2024-25.

Mwanzoni mwa kikao cha ufunguzi, wakurugenzi wasaidizi wakuu wapya watatu wa ILO waliapishwa ambao ni Mia Seppo, mkurugenzi mkuu msaidizi wa ajira na hifadhi ya jamii, Laura Thompson, mkurugenzi mkuu msaidizi wa mahusiano ya nje na biashara, na Hao Bin, mkurugenzi mkuu msaidizi wa huduma za usimamizi wa masuala ya ndani.

Bodi hiyo inakutana katika makao makuu ya ILO Geneva Uswisi kati ya tarehe 13-23 Machi.