Usawa na ujumuishwaji kazini ni chachu ya kujenga mnepo na kujikwamua vyema:ILO

Usawa na ujumuishwaji kazini ni chachu ya kujenga mnepo na kujikwamua vyema:ILO
Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi ulimwenguni, ILO, imebainisha kuwa mtu mmoja kati ya wanne hajisikii kuthaminiwa kazini, huku wale wanaohisi kujumuishwa wakiwa ni wale walioko katika majukumu ya juu zaidi, imeeleza taarifa ya ILO iliyotolewa hii leo mjini Geneva, Uswisi.
Taarifa hiyo ya utafiti inasema viwango vya juu vya usawa, utofauti na ushirikishwaji vinahusishwa na uvumbuzi mkubwa, tija na utendaji, uajiri na uhifadhi wa vipaji, na ustawi wa wafanyakazi lakini uchunguzi wa ripoti uligundua kuwa ni nusu tu ya waliohojiwa walisema kuwa utofauti na ujumuishwaji vilitambuliwa vya kutosha na kufadhiliwa katika utamaduni na mkakati wa maeneo yao ya kazi.
“Ni theluthi moja tu ya makampuni yanayopima ushirikishwaji kwa sasa, ingawa kufanya hivyo ni muhimu kwa maendeleo.” Limesema shirika hilo la kazi duniani.
Tafiti zilizopita
Tafiti za awali kuhusu utofauti na ujumuishwaji zimekuwa zikilenga makampuni makubwa, mara nyingi ya kimataifa, katika nchi za magharibi, zenye mapato ya juu. Ripoti hii mpya, “Kubadili mwelekeo wa biashara kupitia Autofauti na Ushirikishwaji,” inaangazia biashara za ukubwa wa aina zote katika uchumi wa kipato cha chini na cha juu-kati na kukusanya taarifa kutoka kwa mchanganyiko wa watu mbalimbali wafanyakazi, wasimamizi na watendaji wakuu.
Pia inaonyesha aina mbalimbali za umri, jinsia, mwelekeo wa kijinsia, makundi ya kikabila, rangi, dini, watu wenye ulemavu na wale walio na VVU.
Utafiti huo umegundua kuwa hisia ya kujumuishwa mahali pa kazi ina uwezekano mkubwa wa kuhusishwa na ukuu kuliko historia ya kibinafsi au sifa kama vile umri, jinsia au kabila, krangi au dini.
Utafiti umebaini kuwa “asilimia 92 ya wafanyakazi wa ngazi za juu walisema walihisi kujumuishwa, na kwamba utofauti uliheshimiwa na kuthaminiwa kazini, ikilinganishwa na asilimia 76 ya wahojiwa wa kiwango cha chini.”
Pia umesema wafanyakazi katika biashara za ukubwa wa kati, kubwa na za kimataifa pia walikuwa na uwezekano mkubwa wa kujisikia vyema kuliko wale wa biashara ndogo na za kitaifa.
"Usawa katika mahali pa kazi, utofauti na ujumuishwaji ni kichocheo kikuu cha kujenga mnepo na kujikwamua vyema kutokana na janga la COVID-19." Amesema Manuela Tomei, mkurugenzi, Idara ya masharti ya kazi na usawa wa ILO
Ripoti imepongeza kuwa utofauti na ushirikishwaji una jukumu muhimu katika utendaji wa juu wa wafanyikazi, biashara, uchumi na jamii ulimwenguni kote.
"Ikiwa ujumuishwaji unabaki kuwa fursa inayopatikana tu na wale walio katika viwango au nafasi za juu, biashara zinaweza kupoteza fursa ya kupata faida kubwa."

Nafasi ya wanawake na makundi mengine
Ripoti imeonyesha kuwa ni robo tu ya waliohojiwa waliripoti kuwa wanawake walikuwa kundi kubwa (asilimia 40-60) ya wasimamizi wakuu, na theluthi moja walisema hakuna watu wenye ulemavu katika ngazi ya juu.
Baadhi ya vikundi vya wachache pia vimeripoti mara kwa mara matukio machache ya ujumuishi, na vikundi hivi pia vilielekea kujumuishwa katika viwango vya utumishi wa ngazi ya chini zaidi.
COVID-19 imechochea hali kuwa mbaya zaidi
Kwa mujibu wa Manuela Tomei Janga la COVID-19 limefichua na kuzidisha pengo la usawa uliopo katika uchumi na jamii zetu.
Taarifa hizo za utafiti zilikusanywa kati ya Julai na Septemba 2021, wakati wa janga la COVID-19, kutoka kwa wafanyakazi zaidi ya 12,000 katika nchi 75 katika mabara matano.
Theluthi mbili ya washiriki waliripoti kuwa tangu kuanza kwa janga la COVID-19 kiwango cha kuzingatia na kuchukua hatua juu ya utofauti na ushirikishwaji katika maeneo yao ya kazi kimeongezeka.
Lakini sehemu kama hiyo ya watu ilisema janga hilo limeongeza matarajio yao kwa waajiri ya kukuza utofauti na ujumuishwaji.

Haja ya kuhisi kujumuishwa
Ripoti hiyo inasema kwamba njia inayowezekana zaidi ya kushawishi makampuni mengi zaidi kuunda mabadiliko endelevu na ya mageuzi ni kwa kuunganisha biasharana masuala ya utofauti na ushirikishwaji na sera na mifumo ya sheria na maadili ya biashara yanayounga mkono ajenda hiyo.
Ripoti inaainisha kanuni nne muhimu za kufikia mabadiliko na mabadiliko endelevu ambayo yanatumika duniani kote na kwa vikundi na viwango vyote vya wafanyikazi:
Mosi: Utofauti na ushirikishwaji unapaswa kuwa kipaumbele na sehemu ya mkakati na utamaduni;.
Pili: Lazima kuwe na tofauti katika usimamizi wa juu;
Tatu: Viongozi wakuu, wasimamizi na wafanyikazi lazima wawajibike kama mifano ya kuigwa;
Na nne: hatua lazima zitumike katika muda wote wa ajira ambazo zinazohusu uajiri, uhifadhi na maendeleo.