Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima tuchukue mtazamo mpya kwa ajili ya mustakabali wetu wa kimataifa: Guterres

 António Guterres
Video Capture
António Guterres

Lazima tuchukue mtazamo mpya kwa ajili ya mustakabali wetu wa kimataifa: Guterres

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi umezindua mipango mipya ya sera ili kuhakikisha jumuiya ya kimataifa inatekeleza ahadi zake leo, kwa vizazi vijavyo, na kuhakikisha kwamba ulimwengu uko tayari kuchukua hatua ipasavyo kukabiliana na mshituko kama janga la COVID-19.

Muhtasari huu wa sera ya matarajio umeandaliwa ili kuingia katika mashauriano ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchambua jinsi mfumo wa kimataifa unavyoweza kuimarishwa kwa ulimwengu wa kesho, amesema mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, akizindua hivi karibuni nyaraka ya mkakati huo, katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York.

"Lengo ni rahisi", amesema, ni "kuweka maisha mapya katika mfumo wa kimataifa ili uweze kutekeleza ahadi za mkataba wa Umoja wa Mataifa na ajenda ya mwaka 2030.”

Wajibu kwa ushirikiano wa kimataifa

"Jinsi ulimwengu wetu unavyozidi kuwa mgumu zaidi, usio na uhakika, na hatari zaidi, tuna jukumu kubwa zaidi la kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa", ameongeza Guterres, akitarajia mkutano wa kilele wa mustakbali wetu unaotarajiwa mwaka ujao, na mkutano wa Baraza Kuu wa SDG utakaofanyika  Septemba, ambao ameuelezea kama "tukio kubwa la mwaka 2023".

Katibu Mkuu amesema mikutano hiyo miwili mikubwa ni "wakati muhimu kwetu kukusanyika pamoja katika maamuzi muhimu ili kuurejesha ulimwengu kwenye mustakabali wa haki, jumuishi na endelevu kwa wote."

Nchi wanachama zitaamua juu ya upeo wa mkutano huo mkubwa wa wakati ujao, , na mapendekezo yatakayotokana nayo ambayo yataingia kwenye mkataba mpya na wenye dira kwa ajili ya mustakbali wa wote, ameainisha mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Kwa ujumla, muhtasari wa sera 11 utatolewa katika miezi ijayo, zote zikiwa na jicho la kupata dira ya Ajenda Yetu ya Pamoja, na kutengeneza "mfuko kabambe na jumuishi wa mawazo na mapendekezo kwa ujumla.”

Kila sera moja itaeleza jinsi mawazo na mapendekezo yatakavyochangia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), yenye mada muhimu za masuala ya jinsia na haki za binadamu.

Kutafakari na kuchukua hatua kwa ajili ya mustakbali

Bwana Guterres amesema kuweka jicho wazi juu ya siku zijazo, ni kipengele muhimu cha kufikia malengo ya SDGs katika siku zijazo hadi mwaka 2030.

Muhtasari wa kwanza wa sera, Kutafakari na kuchukua hatua kwa ajili ya vizazi Vijavyo, "unaweka wazi kuwa mustakabali salama na wenye usawa unaanza sasa."

Amesema “jumuiya ya kimataifa inakosa mifumo na mikakati ya kivitendo, kugeuza ahadi hizi kuwa ukweli."

Ameongeza kuwa "Kama tungechukua hatua kuzuia na kumaliza utoaji wa gesi chafuzi miaka thelathini iliyopita, janga la mabadiliko ya tabianchi lisingekuwa la kutisha sana leo. Ikiwa tungechukua hatua za kujiandaa kwa magonjwa ya milipuko, janga la COVID-19 lisingeacha zahma kubwa hivi. Kuzingatia mustakbali wetu kuna faida kwa sasa".

Hatua tatu muhimu

Muhtasari huo wa sera unapendekeza hatua tatu madhubuti za kuzingatia, zikichochewa na mipango ya sasa ya kitaifa.

1) Uteuzi wa mjumbe maalum atakayekuwa sauti ya kimataifa kwa vizazi vijavyo, ili "kuongeza ufahamu juu ya athari zitakazowakabili kutokana na maamuzi tunayochukua leo."

Ameongeza kuwa mjumbe huyo wa Vizazi Vijavyo, anaweza pia kutumia manufaa ya mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa.

 2) Mawazo ya kuarifu tamko la kisiasa, ambalo linafafanua "wajibu wetu kwa siku zijazo."

3) Kuundwa kwa kongamano maalum litakalojumuisha serikali mbalimbali, ambapo nchi zinaweza kuendeleza tamko hilo, "na kubadilishana uzoefu na ubunifu."

Katibu Mkuu amehitimisha kwa kusema kwamba “Jukwaa hili litakuwa fursa kwa vizazi kutafakari na kuelezea mshikamano wa vizazi. Kwa hiyo muhtasari wa sera unapendekeza kuundwa kwa Tume ya Vizazi Vijavyo kama chombo tanzu cha Baraza Kuu".