Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi lazima wawajibike kuhusu suala la ufisadi:Guterres 

Umoja wa Mataifa unasema ufisadi ni hatia, ukosefu wa nidahmu na usaliti wa imani ya umma.
UN News/Daniel Dickinson
Umoja wa Mataifa unasema ufisadi ni hatia, ukosefu wa nidahmu na usaliti wa imani ya umma.

Viongozi lazima wawajibike kuhusu suala la ufisadi:Guterres 

Masuala ya UM

Ufisadi ni uhalifu, ukiukaji wa maadili na usaliti wa hali ya juu kwa imani ya umma amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika taarifa yale iliyotolewa leo kuhusu ufisadi na janga la corona au COVID-19.

Katika taarifa hiyo Guterres amesema athari za ufisadi zinakuwa mbaya zaidi hasa wakati kunapokuwa na migogoro kama wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na janga la COVID-19 .“Hatua za kupambana na virusi hivyo zinatoa fursa mpya za kutumia uangalizi dhaifu na kutokuwepo kwa uwazi, kupeleka fedha mbali na watu katika wakati ambao wanazihitaji zaidi. Serikali zinaweza kuchukua hatua haraka bila kuhakiki wauzaji au kubaini bei nzuri.” 

 Ameongeza kuwa wafanyabiashara wasio waaminifu wanatengeneza bidhaa zenye kasoro kama vile mashine za kusaidia kupumua zenye hitilafu, vipimo visivyokidhi viwango au dawa bandia. 

Pia amesema ushirikiano kati ya wale wanaodhibiti minyororo ya usambazaji umesababisha kuwa na gharama kubwa za bidhaa zinazohitajika zaidi, kutapeli soko na kuwanyima wengi matibabu ya kuokoa maisha. 

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesisitiza ,“Lazima tushirikiane kukomesha wizi na utapeli kama huu kwa kubana mtiririko haramu wa kifedha na maficho ya ushuru, kupambana na maslahi ya wanaofaidika kwa njia za usiri na ufisadi na kuwa na umakini mkubwa wa jinsi rasilimali zinavyotumika kitaifa. Kwa pamoja lazima tuunde mifumo thabiti zaidi ya uwajibikaji, uwazi na uadilifu bila kuchelewa. Lazima tuwajibishe viongozi na wafanyabiashara lazima wachukue hatua za uwajibikaji.” 

Guterres ameongeza kuwa kwa muda mrefu ufisadi ni donda ndugu litaweka hatarini malengo ya maendeleo endelevu, SDGs  lisiposhughulikiwa. “Kwa watu wengi katika kanda zote ufisadi kwa muda mrefu umekuwa chanzo cha kutoaminiana na hasira dhidi ya viongozi na serikali zao. Lakini ufisadi wakati wa COVID-19 unauwezekano mkubwa wa kuathiri utawala bora kote duniani na kutusukuma nje zaidi katika kazi yetu ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu.” 

Ametoa wito wa mshikamano kwa viongozi na serikali zote kulitokomeza jinamizi hili kwa faida ya kila mtu.