Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanafunzi wa Afghanistan wahamia Rwanda kuendelea na elimu ya juu

Wasichana wa Afghanistan wanawasili nchini Rwanda kuendelea na masomo.
IOM/Robert Kovacs
Wasichana wa Afghanistan wanawasili nchini Rwanda kuendelea na masomo.

Wanafunzi wa Afghanistan wahamia Rwanda kuendelea na elimu ya juu

Utamaduni na Elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM linasaidia kuhamishia nchini Rwanda, wasichana kutoka Afghanistan ili waweze kuendelea na elimu, kufuatia uamuzi wa serikali iliyojiweka madarakani nchini mwao kupiga marufuku wanawake na wasichana kuendelea na elimu ya sekondari na ya juu nchini Afghanistan. 

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo katika miji ya Geneva, Uswisi na Kigali, Rwanda inasema wasichana hao ni miongoni mwa wanafunzi wa kwanza kutoka nje Rwanda kukubaliwa kujiunga na Shule ya Uongozi ya Afghanistan, SOLA. 

Wasichana wa Afghanistan wanawasili nchini Rwanda kuendelea na masomo.
IOM/Robert Kovacs
Wasichana wa Afghanistan wanawasili nchini Rwanda kuendelea na masomo.

Fahamu SOLA 

SOLA ni shule ya bweni ya wasichana ambayo awali ilikuwa na makao yake kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, lakini ililazimika kuhamia Rwanda kufuatia marufuku ya watalibani. 

Ikiwa ni shule ya kwanza ya aina yake, SOLA inatoa mazingira salama kwa wasichana wa Afghanistan kupata elimu ya sekondari kwa dira ya kujenga kizazi cha viongozi wanawake. 

“Kujituma na uthabiti wa wanawake na wasichana wa Afghanistan katika mazingira magumu, kunatupatia hamasa na kutufanya tuwe wanyenyekevu kila uchao,” amesema António Vitorino, Mkurugenzi Mkuu wa IOM. 

Ameongeza ya kwamba mpango huo wa kuwahamishia SOLA kunamuongezea matumaini ya azma ya kuendelea na uchechemuzi sambamba na wanawake na wasichana nchini Afghanistan kwa ajili ya taifa ambalo linatambua, linasongesha na na kuimarisha mchango wa wanawake na kuwekeza kwa wasichana. 

Kuwasili kwa wasichana hao nchini Rwanda kunafuatia makubaliano kati ya IOM na SOLA wa kusaidia taratibu za kusafiri kwa usalama na usafiri wa wanafunzi hao kutoka nchi ambazo walikuweko hivi sasa baada ya kuondoka Afghanistan hadi kwenye makazi yao katika shule ya SOLA nchini Rwanda. 

Wenyeji nchini Rwanda wakiwakaribisha wasichana kutoka Afghanistan.
IOM/Robert Kovacs
Wenyeji nchini Rwanda wakiwakaribisha wasichana kutoka Afghanistan.

Safarini msichana alipewa kofia ya rubani 

Wanafunzi waliowasili walisindikizwa na maafisa wa IOM hadi kampasi ya SOLA. 

“Wanafunzi walifurahi sana kusafiri kuelekea shuleni kwao. Wakiwa kwenye ndege, msichana mdogo zaidi alipatia kofia na miwani ya rubani. Alifurahi mno na alivalia kofia hiyo safari nzima na kunieleza kuwa akiwa mkubwa anataka kuwa rubani,” ameeleza mfanyakazi wa IOM aliyesindikiza wasichana hao. 

Muasisi wa SOLA Shabana Basij-Rasikh akitathmini makubaliano kati ya serikali ya Rwanda na SOLA ameesma mwezi huu wa Machi mwaka 2023 ni mwaka mmoja tangu watalibani wafunge milango ya elimu kwa wasichana Afghanistani na kuwanyima wasichana haki ya kuendelea na masomo baada ya darasa la 6. 

“Ina maana kubwa sana kwangu ya kwamba hivi sasa wanawasili Rwanda kuendelea na elimu yao na sitachoka kushukuru IOM kwa kusaidia kufanikisha wanafunzi hawa kusafiri salama hadi hapa shuleni ambako watakua na kisha baadaye watakuwa viongozi wa kusaidia kujenga upya Afghanistan,” amesema Shabana. 

Wanafunzi hawa wapya wataungana na wenzao wa SOLA ambao walikaribishwa na serikali ya Rwanda mwezi Agosti mwaka 2021. IOM itaendelea kusaidia uhamishaji zaidi wa wanafunzi wa Afghanistani kuelekea SOLA.