Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana wa Afghanistani waliozuiwa kusoma nchini mwao, sasa washamiri Rwanda

Wasichana wa Afghanistan walipowasili nchini Rwanda kuendelea na masomo. (Maktaba)
IOM/Robert Kovacs
Wasichana wa Afghanistan walipowasili nchini Rwanda kuendelea na masomo. (Maktaba)

Wasichana wa Afghanistani waliozuiwa kusoma nchini mwao, sasa washamiri Rwanda

Utamaduni na Elimu

Siku 1000 tangu marufuku iliyowekwa na mamlaka nchini Afghanistani dhidi ya wasichana nchini humo kuhudhuria shule za sekondari, zaidi ya wasichana milioni moja wamebaki bila fursa ya kupata elimu, ingawa wenzao 40 waliohamia Rwanda wameendelea na masomo tangu mwanzoni mwa mwaka 2023, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji likiongeza kuwa marufuku ilitangazwa tarehe 18 Septemba 2021.

 

Akizungumza nchini Rwanda, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) nchini humo, Ash Carl, amesema "safari ya wasichana hawa ni ishara ya matumaini, ikionesha kwamba pakiwepo na usaidizi unaofaa, elimu kwa vijana inaweza kustawi hata katika mazingira magumu zaidi.”

Taarifa ya IOM iliyochapishwa kwenye wavuti wa shirika hilo inasema kundi hilo la kwanza la wanafunzi wa kike kutoka Afghanistani liliwasili Rwanda chini ya ushirikiano kati ya shule inayoshughulika na masuala ya wasichana nchini Afghanistan inayojulikana kama SOLA (The School of Leadership, Afghanistan) na IOM. 

Mkataba uliotiwa saini mwaka 2023 kati ya IOM na SOLA, unahakikisha kwamba wanafunzi wapya wanapata msaada wa usafiri kwenda Rwanda kutoka nje ya Afghanistan ili kuendeleza elimu yao katika kambi ya SOLA.

SOLA kimbilio kwa wasichana Afghanistani

Kwa upande wake, Mwanzilishi Msaidizi wa SOLA Shabana Basij-Rasikh  amesema, "katika kukabiliana na changamoto ya wasichana nchini Afghanistan kunyimwa fursa ya kupata elimu, SOLA inasalia kuwa kimbilio la kuendeleza masomo na nyota ya matumaini. Hatupingi tu hadithi ya ukandamizaji; tunaandika ukurasa mpya kwa kila msichana anayejifunza, kuongoza, na kuota amani nchini Afghanistan." 

Basij-Rasikh  amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika wanawake na wasichana wa Afghanistan. 

Ingawa mabadiliko yanaweza kuleta mhemko na hisia kali, wafanyakazi wa IOM wanaosafirisha wanafunzi na jamii ya SOLA hufanya kila linalowezekana kupunguza athari za mabadiliko hayo. 

Mnufaika asimulia mabadiliko kutoka Afghanistani hadi Rwanda

Akirejelea mwaka uliopita, mmoja wa wanafunzi anaeleza jinsi mabadiliko yalivyokuwa kwake. "Kujiunga na SOLA ilikuwa mmoja wapo ya mabadiliko makubwa sana katika maisha yangu. Walinikaribisha katika jamii ya upendo na msaada, iliyojengwa na vijana wa kike ambao wanapenda masomo."

 Jumuiya ya SOLA nchini Rwanda inavyokua, kikundi cha wanafunzi waanzilishi cha zaidi ya wasomi 100 wa kike wa Afghanistan waliowasili mwaka wa 2021 sasa wanachukua jukumu muhimu katika kuwakaribisha na kuwashauri wanafunzi wapya. 

Wanafunzi hawa waanzilishi wamekuwa muhimu sana katika kuunda mtandao thabiti unaowasaidia wanafunzi wenzao katika kukabiliana na mabadiliko na mpito, kwa kubadilishana uzoefu wao wenyewe wa kukabiliana na maisha mapya na changamoto za kimasomo nchini Rwanda. 

Kujitolea kwa kikundi hiki cha wanafunzi waanzilishi kusaidia kundi la wanafunzi linalofuata kunaonyesha ni mfano mwafaka wa ari ya SOLA, ambapo kila mwanafunzi anajitolea kuwasaidia wenzake. Safari yao inaashiria siyo tu mabadiliko ya kutoka eneo moja hadi lingine, bali mabadiliko bayana ya kielimu ambayo yanazidi kuimarisha wao kama viongozi wa baadaye. Hawajazoea tu mazingira yao ya masomo mapya bali pia wamestawi, wakionyesha uthabiti wao na kujitolea kwa kujifunza.

Umuhimu wa elimu kwa wasichana wa Afghanistan vikwazo vikizidi kwa wanawake

Kadiri vikwazo vya haki za wanawake nchini Afghanistan vinavyozidi, wasichana wengi zaidi wa Afghanistan wanasalia kuhitaji elimu. Kufikia sasa, SOLA tayari imepokea zaidi ya maombi 2,000 ya darasa lijalo la 2024 huku wasichana wengi wakijitahidi kupata haki ya msingi ya binadamu ambayo wamenyimwa hadi sasa.

IOM inabakia kujitolea kusaidia njia za mara kwa mara za uhamiaji, na kuthibitisha kujitolea kwa mashirika yote mawili kwa elimu na fursa kwa wasichana wa Afghanistan.

Huku vikwazo kwa haki za wanawake nchini Afghanistan vikiongezeka, wasichana wengi zaidi wa Afghanistan wanabaki na uhitaji wa elimu. Hadi sasa, SOLA tayari imepokea zaidi ya maombi 2,000 ya darasa la mwaka 2024 huku wasichana wengi wakifanya juhudi kubwa kutafuta haki ya msingi ya binadamu ambayo wamenyimwa hadi sasa.

IOM inazidi kutoa msaada wa uhamiaji, ikithibitisha upya dhamira ya kuendeleza elimu na kuwapa fursa wasichana wa Afghanistan.