Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtandao wa intaneti, kundi sogozi na vifaa vinginevyo ni chachu ya elimu bora Rwanda- Mwalimu Kabiligi

Wanafunzi wakiwa darasani huko wilaya ya Kayonza, mashariki mwa Rwanda.
© UNICEF/Habib Kanobana
Wanafunzi wakiwa darasani huko wilaya ya Kayonza, mashariki mwa Rwanda.

Mtandao wa intaneti, kundi sogozi na vifaa vinginevyo ni chachu ya elimu bora Rwanda- Mwalimu Kabiligi

Utamaduni na Elimu

Umoja wa Mataifa unasema kuunganisha kila shule kwenye mtandao wa intaneti ni moja ya mbinu za kupunguza pengo la kidijitali kati ya nchi tajiri na zile masikini, na ni hatua pia ya kutekeleza Ajenda ya Pamoja ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

GIGA, mradi unaotekelezwa kwa pamoja na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto UNICEF na la mawasiliano, ITU, unatekeleza maono hayo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, mathalani huko Rwanda ambako kupitia GIGA pengo la kidijitali linapungua; walimu wanafundisha kwa urahisi, wanafunzi nao wanakuwa wanapata taarifa kwa urahisi na za kisasa.

Shuhuda wa GiGA si mwingine bali Mwalimu Feniace Kabiligi wa shule ya msingi ya Murama wilaya Ruhango, jimbo la Kusini nchini Rwanda ambaye sasa anafundisha kwa kujiamini na wanafunzi wana imani naye.

Mwalimu Kabili anasema awali ufundishaji bila intaneti ulikuwa na changamoto lakini anakumbuka siku ambayo walipata mtandao wa intaneti akisema mambo yalikuwa tofauti.

 Anarejelea kumbukumbu hiyo huku akiunganisha waya wa intaneti kwenye kifaa cha kuhamisha taarifa kutoka kwenye kompyuta mpakato kwenda ubaoni.

Kifaa hicho pamoja na mtandao wa intaneti na kompyuta, ni matokeo ya programu iitwayo GIGA iliyobuniwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto, UNICEF na la mawasiliano, ITU mwaka 2019 kuhakikisha kila shule inaunganishwa na mtandao wa intaneti.

GIGA, mradi unaotekelezwa kwa pamoja na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto UNICEF na la mawasiliano, ITU kwa mashule nchini Rwanda
UNICEF VIDEO
GIGA, mradi unaotekelezwa kwa pamoja na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto UNICEF na la mawasiliano, ITU kwa mashule nchini Rwanda

Kundi sogozi lilisaidia kuongeza uelewa wa wanafunzi

Mwalimu Kabiligi anasema, “ilikuwa changamoto lakini sasa naandaa mipango, mazoezi na kila kitu kupitia kompyuta, tofauti na mchakato wa awali uliotumia muda mwingi kuandika kitu kwa mkono. Na wakati ninafundisha naelekeza kwenye ubao na wanafunzi wanaona, na ninaweza kupata taarifa yoyote kwa intanenti tunayopatiwa na GIGA.”

Kisha janga la coronavirus">COVID-19 likabisha hodi mwaka 2020 na Mwalimu Kabiligi anaendelea,“hakuna aliyelitarajia. Lakini hili lilisababisha nijiulize, nifanye nini ili niweze kupunguza kupotea kwa muda wa kujifunza kwa kuwa hatukutambua ni wakati gani shule zitafunguliwa tena. Hapo ndipo nikaja na wazo la kufungua kundi sogozi kupitia WhatsApp kwa kuwa nilikuwa nina namba za wazazi wa wanafunzi wangu wote.”

Ama hakika hatua hiyo bila shaka ilileta matokeo chanya na Mwalimu Kabiligi anasema kuwa “kundi sogozi la WhatsApp lilikuwa chachu kubwa kwa sababu niliweza kuzungumza na wazazi mara kwa mara na kuwapatia masomo na mafundisho kwa watoto wao ili hatimaye watoto waweze kuendelea kufuatilia masomo yao. Na kulikuwa na mabadiliko kwa wanafunzi wangu kwani walipata matokeo mazuri darasani pindi waliporejea shuleni tofauti na kabla ya janga.”

Mradi wa GIGA unanufaisha pia wasio wanafunzi

Mradi wa GIGA unatumia pia shule kama vituo vya kuwezesha jamii kupata huduma ya intaneti ambapo video ya UNICEF inaonesha watu wasio wanafunzi wakiwa jirani na shule wakitumia simu janja zao kurambaza kwenye mitandao.

Na kwa Mwalimu Kabiligi, yeye anasema pamoja na kwamba ni mwalimu, lakini pia ni mwanafunzi na GIGA inamsaidia kwani “kama mwanafunzi, pindi mhadhiri anapotupatia nyaraka za mtandaoni na taarifa, naweza kuzipata kwa urahisi mtandaoni tofauti na awali ambapo nilihaha kupata taarifa mtandaoni.”

Kutokana na UNICEF na ITU kupitia GIGA kubadili maisha ya walimu, wanafunzi na jamii wilayani Ruhango, sasa mwalimu Kabiligi ana ndoto ya kuanzisha “wavuti wa elimu ambamo kwamo watu wanaweza kurambaza na kujifunza mambo mbalimbali. Kuwa na mtandao thabiti wa intaneti kunanisaidia sana kwa kuwa ninaweza kupata habari na taarifa ninazoweza kutumua ili kujiendeleza.”